Wednesday, July 13, 2016

Watumishi Hewa Chanzo Serikali Kusitisha Ajira Mpya 71,496


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema serikali imelazimika kusitisha ajira mpya za watumishi 71,496 serikalini, mwaka huu hadi pale tatizo la watumishi hewa litakapopatiwa ufumbuzi.

Akifungua mafunzo kuhusu maadili ya viongozi wa umma kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji Ikulu Dar es Salaam jana, Kairuki alisema tangu oparesheni ya kutafuta watumishi hewa ianze hadi sasa watumishi 12,246 wameshaondolewa.

Kairuki alisema tatizo la watumishi hewa nchini bado ni kubwa kwani uzoefu unaonesha kuwa nchi nyingi zilizokumbwa na tatizo hilo, ni asilimia ndogo tu ya watendaji ndio iliyokuwa inawajibika.

Alisema kwa sasa serikali imelazimika kusimamisha masuala mengi ya utumishi wa umma ili ipate taarifa kamili ya aina ya watumishi waliopo, na kwamba ma-DED hao kuhakikisha wanasimamia vyema oparesheni hiyo kwani hadi sasa watumishi hewa waliobainika, takribani asilimia 90 wanatokea katika Serikali za Mitaa.

Aidha, Kairuki alisema pamoja na kugundulika kuwa tatizo la watumishi hewa ni kubwa nchini, pia serikali imebaini kuwepo kwa watumishi watoro wasiotimiza wajibu wao.

“Nawataka mkahakikishe mnawabana hawa maofisa utumishi, haiwezekani kuwepo na tatizo la watumishi hewa kubwa kiasi hiki huku pia kukiwa na tatizo la watumishi watoro, hawa maofisa kwani walikuwa na majukumu gani?” Alihoji Kairuki.

Alisema endapo serikali itabaini kuwa maofisa utumishi hao wamehusika katika matatizo hayo ya watumishi hewa na utoro, wataondolewa mara moja. “Serikali haina mchezo kila ofisa katika eneo lake, awe ofisa elimu, afya na kilimo wafanye kazi zao,” alisema.

Mfanyabiashara Anayedaiwa Kujipatia Milioni 7 Kwa Dakika Afikishwa Mahakamani Na Kusomewa Mashitaka 199


Mfanyabiashara Mohamed Mustapha (anayeongea na simu) na wenzake, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kukabiliana na tuhuma za kuibia Serikali kodi ya Sh milioni 7 kwa kila dakika kwa kipindi kirefu.
 **
Hatimaye mfanyabiashara aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa amekuwa akiibia Serikali takriban Sh7 milioni kwa dakika, amepandishwa kizimbani na wenzake wanne na kusomewa mashtaka 199, wote kwa pamoja.

Mfanyabiashara huyo, Mohamed Mustafa Yusufali na wenzake Alloyscious Gonzaga Mandago, Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif Kabla, walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh15 bilioni.

Katika ya mashtaka hayo, Yusufali maarufu kwa majina ya Mohamedali, Choma au Jamalii anakabiliwa na mashtaka 198 yeye peke yake huku wenzake wakikabiliwa shtaka moja la utakatishaji fedha.

Kutokana na wingi wa mashtaka hayo, waendesha mashtaka wawili; Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai walilazimika kubadilishana ili kuwapa muda wa kupumua.

Kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na shtaka la kutakatisha fedha, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu na kulingana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana.

Baada ya kumaliza kuwasomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Hivyo, Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi anayesikiliza kesi hiyo aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Julai 25, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kabla ya kupandishwa kizimbani, Yusufali alitajwa na Rais Magufuli kuwa ana mashine inayotoa risiti za kielektroniki (EFD) nje ya mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuzisambaza kwa wafanyabiashara wengine, hivyo kujiingizia Sh7 milioni kwa dakika.

Rais Magufuli alieleza kuwa mtandao wake unawashirikisha watumishi wa TRA na Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela), hivyo kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

 Katika mashtaka hayo, Yusufali anakabiliwa na mashtaka 181 ya kughushi, mashtaka 15 ya kuwasilisha nyaraka za uongo, udanganyifu katika kulipa kodi moja, shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh15,645,944,361, huku shtaka moja tu la utakatishaji fedha ndilo likimhusisha na wenzake.

Waendesha mashtaka hao walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akighushi nyaraka za kampuni mbalimbali, kuonyesha kuwa zimesajiliwa na zinaendesha  shughuli zake nchini kihalali wakati akijua siyo kweli.

Pia, walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akiwasilisha nyaraka za uongo TRA.

Kuhusu shtaka la kutakatisha fedha, upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Machi 2011 na Januari 2016, walitakatisha Sh1,895,88500 kwa kujifanya kuwa ni malipo ya  mikopo waliyoipokea kwa watu mbalimbali.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa kati ya Januari 2008 na Januari 2016, mfanyabiashara huyo alifanya udanganyifu katika kuwasilisha kwa Kamishna Mkuu wa TRA taarifa ya uongo ya marejesho ya mapato, hivyo kuikosesha Serikali mapato ya kodi ya VAT zaidi ya Sh15.6 bilioni.

Tuesday, July 12, 2016

Rais Magufuli: Sikuchagua Wakurugenzi Vilaza

RAIS John Magufuli amesema wakurugenzi watendaji (DED) wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji aliowateua hivi karibuni, hakuwachagua kwa kubahatisha wala hakuchagua vilaza.

Pamoja na hayo, Magufuli ametoboa siri ya kuihamishia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) chini ya Ofisi ya Rais kuwa ni baada ya kubaini miaka ya nyuma nafasi za ukurugenzi zilikuwa zinatolewa kwa ushawishi na rushwa.

Rais alisema hayo Ikulu Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya viongozi hao wapya ya kula kiapo cha Uadilifu wa Uongozi wa Umma kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kupatiwa semina ya maadili ya viongozi wa umma.

Alisema tangu awateue wakurugenzi hao kumekuwa na maneno ya chinichini na mitandao ya kijamii, ikidai kuwa wengi wao hawana sifa na kufikia hatua ya kumtaja Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Wilaya ya Itigi mkoani Singida, Pius Shija Luhende kuwa ni mhudumu wa hoteli iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam.

Ma-DED wana sifa za kutosha
“Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwatumikia wananchi na kutimiza ahadi pamoja na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 kwa kipindi cha miaka mitano. Tayari hadi sasa miezi minane imeshapotea, nataka utekelezaji wa ahadi hizi uende kwa kasi ya ajabu… 

“…Sasa kwa kasi hii ninayoitaka siwezi kubahatisha katika uteuzi wa viongozi watakaofanikisha azma hii. Hawa wakurugenzi niliowachagua asilimia 80 wana Shahada ya Uzamili na wengine wana Shahada na uzoefu wa kutosha,” alisisitiza Rais Magufuli.

Kuhusu uteuzi wa Shija, alisema anafahamu kuwa mkurugenzi huyo ana sifa za kutosha kuitumikia nafasi hiyo kwa kuwa ana Shahada ya Uzamili na Stashahada na alikuwa ni mkaguzi wa shule.

“Unajua baada ya hili la mitandao ya kijamii nimejifunza mengi, ukiona adui anakushangilia ukifanya jambo, rudi nyuma ujiulize umekosea wapi lakini ukiona adui yako anakushambulia basi ujue umemtwanga,” alisema Rais Magufuli.

Alisema anafahamu kuwa nafasi ya ukurugenzi wa halmashauri ni muhimu katika kujenga uchumi hasa wa chini ndio maana katika kuwateua viongozi hao, ametumia takribani miezi minne kuwachuja na kuwachambua ili kupata viongozi wenye sifa na vigezo stahili.

Hongo kupata u-DED
Alisema zamani wakurugenzi wengi walikuwa wakipata nafasi hiyo kwa kufanya ushawishi kwa kushirikiana na maofisa wa Tamisemi na kuwahonga fedha.

“Pale Tamisemi kulikuwa na timu imejipanga kufanikisha hili. Nimeshaagiza waziri ahakikishe watu wote waliohusika kwa hili wanaondolewa ndio maana niliamua wizara hii iwe chini yangu kwa makusudi,” alifafanua.

Akizungumzia uwajibikaji wa wakurugenzi hao, alisema fedha nyingi za serikali hupelekwa kwenye halmashauri, eneo ambalo limekuwa na sifa mbaya ya fedha hizo kutumika hovyo bila kuzingatia weledi na maadili.

Alisema ndio maana katika uteuzi wa wakurugenzi hao kati ya wakurugenzi 185 waliokuwapo, wa zamani walioendelea ni 60 pekee na 120 ‘wametemwa’, hali inayodhihirisha kuwa waliobaki ni watendaji wazuri ambapo yeye aliwaita ‘majembe’.

Alisema kila mkurugenzi aliyechaguliwa, atambue kuwa sifa zake zilichambuliwa na Rais mwenyewe. “Ndio maana mimi sitembei, nilikuwa nalala saa sita hadi saa nane usiku, nawafahamu wote kwa sifa hadi majina, ninaamini hawataniangusha,” alisema.

Aliwataka kuhakikisha wanazisimamia vyema fedha za serikali zinazowasilishwa katika halmashauri na kuepuka kuburuzwa, kujipendekeza, kukejeliwa au kutumika vibaya kwa kuingia mikataba na kampuni feki zisizoweza kutekeleza vyema wajibu wake.

Fedha za Mfuko wa Barabara
Magufuli alisema anazo taarifa za baadhi ya wakurugenzi, walikuwa wakishirikiana na mameya, madiwani na wenyeviti wa halmashauri kwa kupitisha na kuingia mikataba na kampuni zilizo na uwezo chini ya viwango katika kutekeleza miradi ya barabara; na matokeo yake miradi mingi haikuwa na mafanikio.

“Nawaambieni mkisimamia maadili hakuna atakayewafukuza kazi. Msijipendekeze kwa mtu kwa sababu hakuna aliyepenyeza majina yenu kwangu hadi mkachaguliwa. Kuna mmoja jina lake lilipenyezwa nikalitupilia mbali,” alisema.

Fedha za elimu bure
Aliwataka kuwa makini na kusimamia vyema Sh bilioni 18.77 zinazotolewa na serikali kila mwezi kwa ajili ya elimu bure katika shule za msingi na sekondari kwa kuhakikisha zinatumika vyema kwa lengo lililokusudiwa.

Alisema wapo wakurugenzi waliokuwa wakizitumia vibaya fedha hizo kwa madai kuwa ni nyingi, huku kukiwa na taarifa za baadhi ya walimu wakuu katika kufanya udanganyifu kwa kuandika orodha ya uongo ya wanafunzi na kuongeza idadi ili wapate mgawo mkubwa wa fedha hizo.

Matumizi ya EFDs serikalini Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliziagiza wizara zote nchini chini ya makatibu wake wakuu na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji na taasisi zote za serikali, kuhakikisha wanaanza mara moja kukusanya mapato yake kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).

“Haiwezekani mfanyabiashara alazimishwe kutumia mashine hizi wakati sisi serikalini tunakusanya mapato yetu bila kutumia mashine za EFDs. Ninawataka nyie wakurugenzi mliopo hapa mkifika katika maeneo yenu mhakikishe halmashauri zenu zinakusanya mapato yake kwa kutumia EFDs,” alisisitiza.

Aidha aliwaagiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanashiriki katika kutimiza ndoto ya Tanzania kuwa taifa lenye kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda kwa kila mmoja kuhakikisha katika eneo lake kunaanzishwa viwanda vidogo.

Kodi ndogo ndogo
Akizungumzia kero na changamoto zinazowakabili wananchi, Dk Magufuli aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kipaumbele chao kikubwa kinakuwa ni kuondoa kero za wananchi hasa wale wenye maisha ya chini.

Alisema watanzania wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu na kuhangaishwa na kodi za ajabu hali iliyochangia kurudisha maisha yao nyuma.

“Unakuta mtu analima mpunga wake, akivuna na kuubeba kuupeleka nyumbani kwa matumizi anadaiwa kodi, mbona wakati analima hamkudai kodi? “Nawaomba mhakikishe kodi za aina hii mnazizuia kwani Serikali hii wakati ikiomba kura ya kuingia madarakani, haikuahidi kutengeneza kero kwa wananchi bali kuziondoa kero hizo,” alisema.

Kutumbua majipu
Aliwaagiza wakurugenzi hao watakapofika kwenye vituo vyao vya kazi, kuhakikisha wanachukulia hatua na kuwaondoa mara moja watendaji walio kwenye mamlaka yao wasiowajibika na wale wanaofanya kazi kwa kujifanya miungu watu.

“Nina taarifa wapo watendaji kata ambao wanajifanya miungu watu, kazi yao kubwa ni kuichonganisha Serikali na wananchi, tumieni madaraka yenu kuwaondoa ila msimuonee mtu. Nataka mkawe mitume kwa niaba ya Serikali,” alisema.

Magufuli alisema amewateua viongozi hao kwa kuwaamini na hatarajii itafika siku atajutia uteuzi wake na kubaini kuwa aliwateua kimakosa.

Makamu wa Rais
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuwa kuhudumia na kusimamia watumishi wa umma na wananchi; na si kuwa watawala.

“Kila mtu ajiulize kwa nini Tanzania kwenye watu takribani milioni 50, lakini ameteuliwa yeye. Someni alama za nyakati na muwatumikie vyema wananchi. Someni pia mazingira ya kazi, simamieni utendaji wenu kwa misingi ya sheria na katiba,” alisema Samia.

Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema nafasi ya ukurugenzi katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji ni sawa na injini ya uwajibikaji, hivyo wanaoshika nafasi hizo wanatakiwa kuwa wachapakazi, waadilifu na wenye kujituma ili serikali na taifa kwa ujumla lifikie malengo yake.

“Nawataka mkifika muanze kwanza kuwafahamu vyema washirika wenu kama vile mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, kamati ya ulinzi na usalama, sekretarieti ya mkoa, wakuu wa idara na watumishi. Zijueni vyema ofisi zenu tambueni maeneo yenu ya kazi,” alisema Majaliwa.

Aidha, alisema halmashauri pamoja na kuendeshwa kwa fedha za serikali pia zina vyanzo vyake vya ndani vya mapato na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kusimamia vyema vyanzo hivyo na ukusanyaji wa mapato yake.

Aliwataka kuwa mstari wa mbele kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo ya Rais likiwemo agizo lake la hivi karibuni la kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari ana dawati.

Ma-DC 
Pamoja na wakurugenzi hao kuapa kiapo cha uadilifu, pia wakuu wa wilaya watatu ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu, Agnes Hokororo (Manyoni - Singida) na Miraji Mtaturu (Ikungi – Singida) walikula kiapo hicho.

Ma-DC hao hawakula kiapo cha uadilifu na wenzao hivi karibuni baada ya kubainika makosa katika uteuzi wa wateule wa awali wa nafasi za wilaya hizo. Hokororo alichukua nafasi ya aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo awali, Fatma Toufiq kutenguliwa kwa kuwa tayari ana wadhifa wa ubunge Viti Maalumu.

Babu na Mtaturu walichukua nafasi hizo baada ya wateule wa awali ambao ni Fikiri Avias Said na Emile Ntakamulenga, kutenguliwa uteuzi wao baada ya kuteuliwa kimakosa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanazisoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Aidha, aliwataka kuhakikisha wanatunza maadili yao kama viongozi wa umma na kutambua kuwa wao na viongozi wa umma kwa saa 24 usiku na mchana hivyo wajiepushe na masuala yatakayowavunjia heshima na kuwaaibisha mbele ya jamii.

“Lakini pia nawahimiza mkumbuke kuwa nyie mtakuwa na siri nyingi za serikali haitopendeza kumkuta mbunge ana nyaraka zilizoandikwa siri za serikali kutoka eneo lako. Moja kwa moja utajibu,” alisema.

Jaji Kaganda alisema amebaini kuwa wateule wengi wa nafasi hizo za wakurugenzi ni vijana na kuwahimiza kuhakikisha hawaleweshwi na madaraka hayo na kujiingiza kwenye matendo ya anasa na kujivunjia heshima.

WAKURUGENZI WATENDAJI WA HALMASHAURI, MIJI, MANISPAA NA MAJIJI 185 WALA VIAPO VYA MAADILI LEO IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manidpaa na Majiji 185 kabla ya hawajakula kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano ulioitishwa  na Rais John Magufuli kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote za wilaya na baadhi ya Wakuu wa  wilaya  ikulu jijini Dar es salaam Julai 12, 2016.
Wakuu wa wilaya za Kongwa Mhe deo Ndejembi (kushoto), Siriel Shaidi Mchembe (DC Gairo) na Mhe. Geoffrey Idelphonce Mwambe (DC Manyoni) wa kila kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukosa kufanya hivyo na wenzao wiki iliyopita. 

Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji 185 wakila kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam.

Kituo Cha Dk. Mwaka Chafutiwa Usajili Wake


Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, limekifutia usajili wake wa kutoa huduma za kitabu, Kituo cha Tiba Asilia cha ForePlan Kliniki kilichopo Ilala Bungoni jijini Dar es salaam, kinachomilikiwa na Dkt. Juma Mwaka maarufu kama Dkt. Mwaka, kwa madai kuwa kimekiuka taratibu za kitabu za tiba mbadala.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dkt. Edmund Kayombo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ukumbi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Akizungumza jijini Dar es salaam leo katika Mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk. Edmund Kayombo amesema kuwa kufutiwa kibali cha Dk. Mwaka kunatokana na sababu nyingi ambazo amekuwa akikiuka licha ya kupewa maonyo na barua juu ya utoaji huduma zake.

Amesema sababu nyingine ni kuwa katika matangazo yake amesema anatoa tiba za kisasa wakati hiyo elimu hana ya kufanya huo.

Wengine waliofutiwa usajili ni Fadhaget Sanitarium kinachoendeshwa na Tabibu Fadhili Kabujanja pamoja na Mandai Herbal Clinic kinachoendeshwa na Tabibu Abdallah Mandai

Hata hivyo limetoa adhabu mbalimbali kwa kituo cha Aman Herbal Clinic kinachoendeshwa na Tabibu Esbon Baroshigwa, na Tabibu Castory Ndulu wa Kituo cha Ndulu Herbal Clinic wamepewa barua ya onyo.

Aidha wengine wamesimashwa kwa miezi sita ambao ni Tabibu John Lupimo wa Lupimo Suntarium Herbal Clinic pamoja na Tabibu Simon Rusigwa wa Sigwa Herbal Clinic.

Wanafunzi Chuo Kikuu Kizimbani Kwa Mauaji Baada ya Kufanya Tukio la Ujambazi katika Benki ya CRDB eneo la Chanika


WATU watatu wakiwemo wanafunzi wawili wa vyuo vikuu vilivyoko jijini Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji.

Wanafunzi hao ni wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Hussein Mustafa (26) na wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Haruna Nkuye (24) ambao wanashitakiwa pamoja na fundi makenika Rajabu Ally (41) wote wakazi wa Dar es Salaam.

Washitakiwa hao wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo kwenye tukio la ujambazi katika Benki ya CRDB eneo la Chanika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, walisomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Jackson Chidunda mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi.

Akisoma hati ya mashitaka, Chidunda alidai Desemba 8, mwaka jana katika eneo la Chanika, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, washitakiwa walimuua Ramadhani Halili, Shan Rajabu na Thomas Otemu.

Hakimu Shahidi alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo isipokuwa Mahakama Kuu.

Upande wa jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili wamuunganishe mshtakiwa Mohamed Ungando ambaye jana hakuwepo mahakamani.

Awali, mshitakiwa Mustafa aliiomba mahakama imsaidie apate matibabu kwa kuwa viungo vinamuuma kutokana na adhabu alizopewa akiwa mahabusu.

Hakimu Shahidi alisema gerezani kuna utaratibu wa matibabu, kama hatatibiwa kesi itakapotajwa tena aijulishe mahakama. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 14, mwaka huu.

Nchi Nyingine ya Afrika Yazima Mitandao ya Kijamiii ya What's app na Facebook..Kisa Inasababisha Wanafunzi Wasisome


Mitandao ya kijamii nchini Ethiopia imezimwa.

Waethiopia waliamka Wikiendi wakajipata hawana huduma hizo za mitandao kama Facebook, Twitter, Instagram na Viber.

Serikali imefunga mitandao hiyo tangu Jumamosi usiku.

Msemaji wa serikali ameiambia shirika la habari la AFP kuwa serikali ilichukua hatua hiyo kama njia ya kuzuia wanafunzi wasivurugwe na ushawishiwa mitandao hiyo ya kijamii.

Hatua hiyo vilevile imetokea majuma kadhaa baada ya baadhi ya makaratasi ya mitihani kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kulazimu serikali kufutilia mbali mitihani hiyo iliyodukuliwa.

''Serikali imechukua hatua hiyo kwa muda hadi siku ya Jumatano.

Tumegundua kuwa mitandao ya kijamii huvuruga kabisa ratiba ya vijana na haswa wanafunzi'', alisema msemaji wa serikali Getachew Reda .

Serikali imechukua hatua hiyo kwa muda hadi siku ya Jumatano mitihani itakapokuwa imekamilika
Hatu hiyo bila shaka imewaudhi wanaharakati wa kupigania uhuru wa habari nchini Ethiopia.

Mwanabloggu mashuhuri Daniel Berhane amechapisha kwenye mtandao wake wa Twitter maswali ambayo anataka yajibiwe.

Je ni nani aliyechukua uamuzi huu?

Aliwashauri kina nani ?

kwanini alichukua hatua hiyo?

Je hii haitakuwa mwanzo wa tatizo lipya la kukandamiza uhuru wa kujieleza ?
Powered by Blogger.