Friday, February 3, 2017

Kutana na Baba Pamoja na Bintiye Wanaotamba Mitandaoni Kwa Kuonyeshana Mahaba Yanayohanikizwa na Urefu wa Nywele Zao za Asili..!!!


NI mwimbaji anayekuja juu, mwandishi wa nyimbo, mwanamitindo na baba wa aina yake, ambaye ni mkazi wa New York na Los Angeles nchini Marekani.

Baba huyu wa mtoto mmoja, Benny Harlem, kwa kipindi kifupi ameweza kuiteka mitandao kama vile Instagram, shukrani zikiendea aina ya nywele zake, kujivunia rangi ya ngozi yake nyeusi sambamba na bintiye mpendwa.

Harlem na bintiye mwenye umri wa miaka sita, Jaxyn daima wameonekana pamoja katika mitandao ya kijamii na hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wengi kwa namna ya mitindo yao inayoendana.

Ni hali iliyowafanya wajichotee mamia kwa maelfu ya wafuasi kutokana na haiba yao hiyo na kuonekana kana kwamba hawatenganishwi angalau kwa sekunde moja.

Jarida la Paper liliwahi kuzungumza naye kuhusu mvuto wao katika intaneti, wanavyolinda mwonekano wa misuli na ukakamavu wake pamoja na weusi wa ngozi yake katika Marekani ya leo na siri ya mafanikio ya nywele zake.

Baba huyu anasema hupenda kuonesha mfano mkubwa kwa msichana wake mdogo katika masuala ya kujiamini na kukumbatia asili yake.

Aidha, kutokana na uzoefu wake wa malezi aliyopitia nyuma, anataka kuelimisha jamii kwa vitendo hasa kwa wababa wenzake kuwapenda watoto wao na kuwapa mwongozo utakaowasaidia maishani.

Benny anasema kazi yake kama mzazi ni kumlinda na kumkuza mtoto wake huku akiwa na matumaini kuwa Jaxyn atakuwa msichana mwenye nguvu na kujiamini.

“Binti yangu ni mzuri na ninatarajia atakuwa mwanamke mrembo, lakini namfundisha ajipende yeye kwanza. Haelekezi macho kwa wanaume, au kuangalia televisheni au marafiki zake.”

Dogo Jaxyn anaonekana kuwa na imani na daima mwenye furaha kwa rangi ya ngozi yake, hivyo huwezi kukana kuwa babake anafanya vyema katika kazi yake ya uanamitindo


Kuhusu siri ya nywele zao, anasema wanaziosha kila wiki, wanatengeneza shampoo na vitu kama hivyo kwa kutumia viungo vya asili kama vile mafuta ya nazi na kadhalika na kuwa hakuna kitu kikubwa zaidi ya hilo na matunzo mazuri.

Anasema binti yake Jaxyn anakumbana na wakati mgumu awapo shule, ambako wasichana hujaribu kuzishika nywele zake.

Kwa vile nyumba ameweka sheria ya kutoruhusu yeyote kugusa nywele zao, bintiye huyo anaendeleza utaratibu huo awapo shuleni, kitu ambacho mara nyingi ni changamoto mno kukizuia.

Anasema; “Watu wanatutazama na  kutuuliza iwapo kweli ni nywele zetu hasa zangu ni za asili au za kupandikiza. Jibu tunalowapa ni ndio. Kwa kweli wengi wameondokea kuzipenda pamoja na kuwa kuna wachache walio kinyume na hilo.

“Naona fahari ya kuwa hivi nilivyo.”

Hata hivyo, Harlem hajapitia mapenzi ya ubaba kama anayoonesha kwa bintiye, kiasi cha kuwa mfano kwa wababa wengi wanaomfuatilia mtandaoni.

Benny (27) ambaye alianza kukuza nywele zake tangu akiwa na umri wa miaka 15 anasema: “Binafsi sikuwahi kukutana na baba yangu hadi nilipokuwa na umri wa miaka saba. Wakati huo baba alikuwa kocha wa mpira wa miguu katika shule ya juu ya sekondari, hivyo mimi na familia yangu––yaani mama, shangazi na bibi yangu tulienda uwanjani na kusubiri hadi mpira ulipomalizika. Tuliingia kiwanjani na shangazi yangu akamwambia baba, ‘Hey! huyu ni mwanao.”

“Baba aliniangalia kwa sekunde 10 na kisha akasema, sina mtoto hapo. Ni kauli ninayoikumbuka sana na iliniuma sana kipindi kile” anasema taratibu kwa vituo kila baada ya maneno machache.

Anasema ni alihisi uchungu wa kukataliwa hasa ukiongeza namna alivyokuwa akiingiwa na wivu wa kuwaona watoto wenzake wakiwa wameshikwa mikono na baba zao matembezini na wanapopelekwa au kurudishwa nyumbani kutoka shuleni.

Baadaye, ili kuziba pengo hilo aliamua kuachana na hilo na kukubali hali halisi. “Nilijitegemeza zaidi kwa wanawake, ambao wametawala katika familia yetu. Nilikulia katika mazingira yenye wanawake watupu na mimi nilikuwa mwanaume pekee katika familia yetu licha ya kwamba nilikuwa na wajomba wachache mno.

“Kwa sababu hiyo niliwachukulia kina David Bowie (mwimbaji na mcheza filamu) na Tupac Shakuru (mwanamuziki wa rap ambaye ni marehemu) kama wababa wangu,” anasema Harlem, ambaye hakuna popote katika mitandao anakozungumzia mkewe au rafiki yake wa kike au kwa maneno mengine mama wa bintiye Jaxyn 

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.