Fikiria kila unachokijua na kukikumbuka kuhusu mabadiliko unayotaka yawe katika maisha yako, halafu uone ukweli huu kama kweli nawe ni mmoja kati ya watu wanaotaka mafanikio au uko nje ya mstari wa mafanikio na pengine tu wewe hujijui. Kama kweli unataka mafanikio, ni kwanini mara kwa mara umekuwa ukisita au kuogopa kufanya jambo ambalo lingeweza kubadili maisha yako na kukuletea mafanikio mkubwa? Hili ndilo tatizo walilonalo watu wengi wanahofia sana kufanya mabadiliko kwa namna moja au nyingine hata kwenye yale malengo waliojiwekea wao wenyewe kuna wakati huwa wanaogopa pia.
Kimaumbile, kila binadamiu anahofia mabadiliko, lakini hofu ya mabadiliko inapozidi kuwa kubwa na kukuzuia kufanya mambo ya maana kwako, hofu hii sasa hugeuka kuwa ni maradhi yanayokuzuia wewe kufanikiwa. Hebu fikiria tena, ni mara ngapi umekuwa ukitaka kufanya mabadiliko Fulani katika maisha yako, lakini umekuwa ukijikuta ukishindwa kufanya hivyo kutokana na kuogopa kufanya vitu Fulani? Ni mara ngapi umekuwa ukitaka kuingia kwenye biashara lakini umekuwa na hofu nyingi zinakuzuia? Hivi ndivyo ilivyo mabadiliko huogopwa, wakati mwingine bila sababu ya msingi.
Wengi wetu kutokana na kuogopa mabadiliko, hujikuta ni watu wa kutoa sababu ambazo hata hazina mashiko zinazosababisha wao washindwe kutekeleza malengo na mipango waliojiwekea. Utakuta mtu anakwambia hawezi kufanya biashara ni kwa sababu hana mtaji, ukija kuchunguza kidogo utagundua kuwa hiyo ni sababu ambayo amekuwa akiitoa kwa muda mrefu, iweje kila siku mtu huyohuyo awe hana mtaji tu. Kama uko hivi una hofu tu hata kwa vitu vidogo ambavyo ungeweza kuvifanyana , tambua kuwa kuanzia sasa unaye adui mkubwa ndani mwako anayekuzuia kufanikiwa. Na unapoogopa kufanya mabadiliko ambayo unaahitaji sasa ili ufanikiwe, sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako yote.
Tatizo kubwa utakalokuwa nalo linalosababishwa na hofu hii ya kuogopa kufanya mabadiliko ni lazima utakuwa mtu wa kutaka mafanikio ya harakaharaka. Watu wengi wenye mawazo ya kutaka kufanikiwa leoleo hata kama wameanza biashara leo, wengi wao huwa wana hofu hii kubwa ya mabadiliko ndani mwao, unaweza kufanya utafiti mdogo utagundua ukweli huu ulio wazi. Hawa ni watu ambao kiuhalisia hawaijui wala kuiamini subira ndani mwao, bali ni watu wakutaka mfumo wa maisha uwe ambao unaanza leo biashara na wiki ijayo uwe tajiri ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa.
Hivi ndivyo walivyo watanzania wengi wanaogopa mabadiliko na kuamini katika miujiza, sio katika wao wenyewe kutenda na kuona matokeo. Hebu jaribu kukagua maisha ya walio wengi utakuja kugundua ukweli huu ni watu wanaofikiria sana leo, sasa hivi, siyo baadaye. Hata malengo yao ni ya karibu sana na hawataki shida, wanataka wafanye leo, wamudu leo na kila kitu kimalizike leo. Sijui kesho watafanya kitu gani? Ukimwambia mtanzania aanzishe mradi ili aje faidi baada ya miaka 10 kutoka sasa kwanza atakushangaa, kisha atakucheka we hadi mbavu zimuume. Anataka leo hata kama ni kwa miujiza.
Ndiyo maana wengi kati ya Watanzania hawana malengo, wanaishi tu na kutawaliwa na hofu za mabadiliko. Kuweka malengo siyo sehemu ya maisha yao, kwani malengo yanataka mtu mwenye subira, mtu anayeamini kwamba maisha ni kuanguka na kusimama. Wanachojua kikubwa ni kulalamika na kulaumu, kuponda na kukejeli, kwa sababu wao wamekata tamaa bila kujijua. Ndiyo maana ni watanzania wanne tu kati ya kumi ambao wanafanya kazi, wanatoka jasho na wanaweza kusubiri bila kukata tamaa, wengine waliobaki wanasubiri ujanja ujanja tu ilimradi wafanikiwe hata kama ni kwa kufanya uhalifu wa aina yoyote.
Ni watu ambao wanataka kuishi kihadithi, wawe na pete ambayo wanaweza kuiamuru iwape wakitakacho na wakipate. Maisha ni ya kibunuasi- abunuasi tu, watu hawa kwao mabadiliko ni kitu kigumu sana kwao na kinaogopwa kweli. Kama unataka mafanikio ya kweli yawe kwako, unatakiwa kubadilisha fikra za zako na kuamua kukubali kuwa mafanikio yanahitaji mabadiliko makubwa sana ambayo wewe mwenyewe unatakiwa uyafanye kwa kujitoa hasa. Acha kuwa na hofu zisizo na maana zinazokuzuia wewe usifanikiwe, chukua hatua katika maisha yako, kuyafikia maisha unayoyataka