Mheshimiwa Rais,
Mimi ni Raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninakupongeza sana kwa kazi nzuri unayofanya kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Tanzania wanafaidi matunda ya Uhuru.
Mheshimiwa Rais,
Ninakupongoza na ninakuombea kwa Mwenyezi Mungu ili uendelee kutimiza ahadi yako ya kutumbua majipu kwa kupambana na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na ufisadi nchini kama ulivyolitangazia Taifa kupitia Bunge tarehe 20-11-2015. Ni imani yangu kuwa kama ulivyoahidi katika hotuba yako, ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma na rushwa serikalini vitageuka kuwa wimbo uchukizao badala ya wimbo ufurahishao kama ilivyokuwa imezoeleka hapo awali.
Mheshimiwa Rais,
Pia ninapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza na kumwombea Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kazi nzuri sana anayofanya. Kadhalika napongeza watendaji wote uliowateua kuunda Serikali yako katika Wizara mbalimbali ili kukusaidia kufanikisha malengo yako ya kuleta hali bora zaidi kwa wananchi wote wa Tanzania katika maisha yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Rais,
Ni vigumu kuweza kutimiza ahadi yako ya kupambana na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na ufisadi nchini kama hutapata taarifa sahihi za ni nini kinatendeka katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kama Raia wa kawaida tunao wajibu wa kutoa taarifa sahihi za kila jambo lisilo la kizalendo lenye nia ya kuharibu ustawi wa jamii na Taifa.
Kwa mujibu wa Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni wajibu wa kila mtu kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Rais,
Chuo cha Ufundi Arusha ni mali ya Mamlaka ya Nchi. Chuo hiki kina dhamana ya kutoa mafunzo bora kwa wananchi wote wa Tanzania. Katika kutekeleza majukumu yake, chuo kimekumbwa na matatizo mbalimbali. Miongoni mwa matatizo yaliyopo ni upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, upungufu wa malazi kwa wanafunzi, Ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Rais,
Kutokana na upungufu wa malazi wanafunzi wengi wa kike wanakaa nyumba za kupanga mitaani. Matokeo yake wanafunzi wengi wamepata ujauzito na wengine wengi wameshindwa masomo yao kwa kukosa mazingira rafiki ya kujisomea. Wanafunzi wanaoathirika zaidi ni wanafunzi wanaosoma ngazi ya cheti na stashahada ambao wengi wanatokea kidato cha nne (4) na wengi wana umri wa chini ya miaka 18.
Mheshimiwa Rais,
Chuo kingeweza kuondokana na tatizo la upungufu wa malazi kama kungekuwa na nia hiyo. Chuo kilikuwa na matofali zaidi ya 20,000, Chuo kinapata simenti kutoka kiwanda cha Tanga simenti na wanafunzi huwa wanafanya mazoezi ya kujifunza kujenga chuoni. Ni kiasi kidogo sana cha rasilimali fedha kingeweza kutumika kuondokana na tatizo la malazi chuoni.
Mheshimiwa Rais,
Chuo huwa kinapata msaada wa simenti tani nane (8) kila muhula kwa ajili ya kuendesha mafunzo kutoka kiwanda cha Tanga simenti. Kadhalika chuo kilikuwa na matofali zaidi ya 20,000 yaliyopigwa chuoni na kubaki katika ujenzi wa jengo la Ujenzi na Umwagiliaji. Kutokana na mazingira yasiyoeleweka, haifahamiki inakokwenda simenti hii ya msaada na pia haikufahamika yalikokwenda matofali yale yote.
Inavyoonekana tatizo la malazi liliachwa na kuwa kubwa ili serikali iweze kutenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni. Kutengwa kwa fedha za ujenzi wa mabweni kungeweza kupelekea kufujwa kama ilivyokuwa kwa miradi mbalimbali ya ujenzi iliyofanyika chuoni kuanzia Januari 2010. Chuo kimekua kikifuja fedha nyingi za umma kupitia kampuni ya chuo ijulikanayo kama ATC-PCB.
Mheshimiwa Rais,
Chuo cha ufundi Arusha kina njia mbalimbali za mapato, lakini kwa sasa chuo kinaendeshwa kwa madeni. Upande mmoja wafanyakazi wanadai chuo stahili mbalimbali na kwa upande mwingine wazabuni/wafanyabiashara nao wanadai chuo mabilioni ya fedha kwa huduma mbalimbali walizotoa kwa chuo. Sintofahamu inazidi zaidi pale ambapo haijulikani madeni haya yatalipwa lini na ni nini ilikuwa msingi wa madeni haya.
Mheshimiwa Rais,
Kutokana na matumizi yasiyoridhisha ya fedha za chuo, hata wanafunzi wa kozi ya Ujenzi na Umwagiliaji wameshindwa kufanya mazoezi yao inavyostahili. Wanafunzi hao wameshindwa kufanya mafunzo yao sawasawa kwa kukosekana eneo la kufanyia mazoezi (Practical practice). Wanafunzi hawa walitakiwa kuanza kufanya mazoezi hayo kwenye shamba darasa lililopo eneo la Oljoro tangu mwaka 2013.
Wafadhili mbalimbali walitoa fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya shamba hilo. Inakadiriwa kuwa kiasi cha TZS 400,000,000/= kilitolewa na wafadhili kwa ajili hiyo lakini mpaka sasa wanafunzi hawajaweza kufanya mazoezi katika shamba hilo na haijulikani ni lini wataanza kufanya mazoezi kwenye shamba hilo. Kwa sasa shamba hilo limegawanywa kwa baadhi ya wafanyakazi wa chuo kwa lengo la kujilimia.
Mheshimiwa Rais,
Katika mazingira yenye utata baadhi ya watumishi wa chuo walijilipa mishahara binafsi kuanzia Juni 2010 na haifahamiki ni mamlaka gani zilizowapa mishahara hiyo. Wapo wafanyakazi/watendaji wenye mishahara binafsi serikalini lakini huwa inafahamika ni mamlaka gani zimewapa watendaji hao mishahara hiyo. Kwa mtizamo huo, imefikiriwa kwamba pengine mishahara hiyo ilipatikana kwa njia ya kutumia madaraka vibaya, au kwa kujuana au kwa kuangalia sura zaidi ya sifa ya mtumishi husika. Hali hii imezua manung’uniko na huenda ari ya kazi imeshuka kwa baadhi ya watumishi na pengine utafiti ungefanyika leo ungeweza kuonesha kwamba tija chuoni imeshuka.
Mheshimiwa Rais,
Chuo cha Ufundi Arusha kimekuwa na bahati ya kupata vibali vingi vya ajira tangu mwaka 2010 hadi sasa. Serikali kwa nia njema imetaka kuboresha utendaji wa chuo kwa kukiongezea nguvukazi/rasilimali watu. Ni dhamira ya Serikali pia kupunguza tatizo la ajira kwa watanzania kwa kutengeneza nafasi nyingi za ajira iwezekanavyo. Pia ni matumaini ya serikali kuwa ajira zinazopatikana zitashindanishwa kwa haki kwa watanzania wote wenye sifa. Tofauti yake, kwa nyakati tofauti chuo kimetangaza nafasi za ajira lakini sehemu kubwa ya nafasi hizo huwa tayari zina wenyewe na hatimaye waliajiriwa.
Mwezi Februari 2016 chuo kilitangaza nafasi za ajira. Katika nafasi hizo imefahamika kwamba sehemu kubwa tayari zina wenyewe. Zitakazobaki zitaendelea kujazwa kidogo-kidogo hadi mwaka 2017. Imepangwa hivyo ili baadhi ya walengwa wa viongozi wa chuo watakapokuwa wamemaliza masomo yao kutoka vyuo mbalimbali wanavyosoma hivisasa wawe wamemaliza masomo yao. Walengwa hao tatajaza nafasi hizo kwa njia ya kujaza nafasi ambazo mara nyingi zinaitwa “hazikupata watu wenye sifa” na hivyo kuendelea kutangazwa tena na tena mpaka watakapofika.
Mheshimiwa Rais,
Chuo cha Ufundi Arusha kwa sasa hakina Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji. Kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Chuo cha Ufundi Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ni mteule wa Rais. Imekuwa kama ni kawaida sasa kwa Bodi ya Uendeshaji kukutana na kufanya vikao vya Bodi na kulipana posho bila kuwepo Mwenyekiti wa Bodi na bila kibali cha Waziri kama itabidi kufanya hivyo na haifahamiki ni kwa nini.
Mheshimiwa Rais,
Mara nyingi Serikali imekuwa ikikaangwa kwa mafuta yake yenyewe kwani baadhi ya watendaji wasiowaaminifu wamekuwa wakihongwa kwa fedha zilizopatikana kifisadi kuachia mafisadi kuendelea kuteketeza rasilimali za nchi.
Mheshimiwa Rais,
Haijawezekana kukuona ana kwa ana na pia haikuwezekana kukufikishia barua hii kwa njia nyingine. Lakini inafahamika kwamba Serikali ina mkono mrefu na kwa hivyo barua hii itakufikia. Juhudi kubwa imefanyika kuweza kukufikishia barua hii Mheshimiwa, ili uweze kupata taarifa sahihi za ni nani, anafanya nini, na yuko wapi.
Mheshimiwa Rais,
Mimi na Watanzania wengi wenye mapenzi mema tunakuombea maisha yenye Heri na Baraka wewe na wasaidizi wako wote katika Serikali yako.
Wako mtiifu,
Subira – Mtanzania MzalendoLast edited by SUBIRA; Yesterday at 22:56.
BLOGU YA LEWIS MBONDE BLOG YASITISHA KUTOA MAUDHUI MTANDAONI
-
Kutokana na matakwa ya kisheria ya maudhiu ya kutoa huduma za kimtandao
bila kuwa na leseni iliyotolewa na mamlaka ya udhibiti wa huduma za
mawasiliano t...
6 years ago
0 comments:
Post a Comment