JESHI la Polisi Zanzibar limetoa tahadhari kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wanaitumia kwa kuwatukana viongozi wa kitaifa, huku likiwa na orodha ya watu 34 ambao wanatarajiwa kuhojiwa zaidi kutokana na matumizi mabaya ya mitandao hiyo.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Salum Msangi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.

Alisema hivi sasa baadhi ya watu wanaitumia mitandao hiyo kinyume na maadili jambo ambalo linaweza kusababisha chuki na uhasama na kwamba ni kinyume na maadili ya wananchi wa Unguja na Pemba.

Msangi alisema jeshi hilo linakusudia kuwahoji watu 34 wanaotumia mitandao hiyo ya kijamii kwa kuhamasisha vurugu pamoja na kutoa lugha za matusi kwa viongozi wa Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume na sheria pamoja na utamaduni wa wananchi wa Zanzibar.

Alisema mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, kumejitokeza baadhi ya watu na vikundi mbalimbali vinavyotumia mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno ya matusi au kutoa video za kuzungumza zenye lugha ya matusi kwa kuwatukana watu mbalimbali hasa viongozi wa kitaifa.

“Tayari orodha ya watu hao imeshapatikana na hadi sasa Polisi inamshikilia kwa mahojiano na uchunguzi mtu mmoja ambaye anatuhumiwa kutoa moja ya video hizo zenye lugha ya matusi dhidi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein,” alisema.

Aidha alisema kuwa uchunguzi wa kitaalamu na kisayansi unaendelea na ukishakamilika jalada litafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulisoma na kulifikisha kwenye hatua zinazofuata.

Msangi alitoa tahadhari kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani kutumia lugha za matusi ni kosa lililoainishwa kisheria kwenye sheria ya kanuni ya adhabu, yoyote atakayetenda kitendo hicho atakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, bila ya kujali limetolewa mahali gani au wakati gani.

Hata hivyo alisema kuwa wapo watu wanaodhani kuwa demokrasia ni uhuru wa kuwatukana viongozi, jambo ambalo sio sahihi na halikubaliki kisheria na kinyume na maadili ya wananchi wa Tanzania ambao wamejengwa na utamaduni wa kuheshimu watu.

Msangi ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar, alisema orodha ya watu wanaojiuhusisha na vitendo hivyo wanayo na wataendelea kukamatwa mmoja baada ya mwingine na kuchukuliwa hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein alikemea tabia iliyojitokeza sasa ya matumizi mabaya ya mitandao.