Saturday, December 24, 2016

WASICHANA 21 wa Chibok Waachiliwa Huru



Wasichana 21 kati ya wasichana 276 waliotekwa nyara na Boko Haram walipovamia shule mnamo 2014 .

Wasichana 21 wa Chibok waachiliwa huru

Msemaji mkuu wa rais Garba Shehu alifahamisha kwa taarifa kuwa wasichana 21 wameachiliwa huru.

Aidha taarifa pia zafahamisha kuwa watu wasiopungua 2000 wameokolewa kutoka wilaya ya Borno nchini Nigeria .

Hata hivyo wasichana walio chini ya Boko Haram bado haijulikani walipo .

SERIKALI Yapiga Marufuku Shule Binafsi Kufanya Mitihani ya Kuchuja Wanafunzi



Hiyo ni baada ya kutangaza kupiga marufuku utaratibu wa kuwachuja wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani ya taifa uliokuwa unaofanywa na baadhi yao kwa lengo la kuonekana shule zao zinafaulisha vizuri.

Hivi karibuni, Nipashe iliripoti kuhusu hofu ya baadhi ya shule hizo; za msingi na sekondari ziko hatarini kubadilishwa matumizi kutokana na kukosa wanafunzi wa kutosha baada ya Serikali kuboresha shule zake na kutoa elimu bure, huku hali ya kiuchumi ikiwaumiza wananchi.

Huku udahili kwenye shule za serikali ukiongezeka na kuonekana kuwa tishio kwa ustawi wa shule za watu na taasisi binafsi, imewabana tena wamiliki wa shule binafsi kwa kuwazuia kufanya mchujo wa wanafunzi wanaoingia kwenye madarasa au vidato vyenye mitihani ya taifa.

Mmoja wa wazazi aliliambia Nipashe kuwa mwanawe anayesoma kidato cha tatu katika shule moja ya binafsi jijini Dar es Salaam, amepangiwa kuhamishiwa shule nyingine ya mmiliki huyo huyo kutokana na kufaulu kwa daraja la tatu.

Kwa mujibu wa mzazi huyo, kuna wanafunzi takribani 70 wa kidato cha tatu, wanatarajiwa kuhamishwa katika shule hiyo waliyosajiliwa tangu kidato cha kwanza, watahamishwa shule hiyo na kubaki wale waliofaulu kwa viwango vya madaraja ya kwanza na pili tu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, alisema ni marufuku shule kumkaririsha darasa, kumfukuza, kumhamishia shule nyingine au kumsajili kama mtahiniwa binafsi (PC) mwanafunzi kwa kigezo cha kutofanya vizuri katika mitihani ya shule husika.

"Ni marufuku kabisa kufanya hivyo. Mitihani tulionayo sisi (Wizara ya Elimu) ndiyo mchujo sahihi. Na mtihani ambao unamkaririsha mwanafunzi ni mtihani wa taifa wa kidato cha pili na mtihani wa darasa la nne tu," alisema.

"Wala siyo mtihani wa shule na madarasa mengine hayana mtihani wa kumkaririsha mtoto au kumfanya aondolewe shuleni au ahamishiwe shule nyingine, hatuna utaratibu huo na serikali haiwezi kukubaliana nao," aliongeza Dk. Akwilapo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongosco), Benjamin Nkonye, aliiambia Nipashe jana kuwa utaratibu wanaoutumia ni kushauriana na wazazi wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri shuleni ikiwamo kuwapeleka katika vyuo vya ufundi (Veta).

Alisema shule binafsi zinapaswa kupongezwa kwa kudahili hata wanafunzi hasa wa sekondari ambao shule za serikali huwa haziwachukui kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya shule za msingi.

“Hakuna shule ambazo zinapaswa kupongezwa kama za binafsi, serikali yenyewe imekuwa ikichagua wanafunzi wote. Inatuachia ‘vilaza’, lakini sisi kwa kujitoa kuwasaidia watoto wa Kitanzania, tunakubali kuwachukua hao hao wanaoonekana wabaya, tunawafundisha na mwisho wa siku wanakuwa wazuri kuliko hata hao wanaokuwa wamethaminiwa na serikali,” alisema Nkonya.

“Na sisi hatuchuji wala kumfukuza mwanafunzi, isipokuwa kinachofanyika kwa kuwa tunapokea wakati mwingine wanafunzi ambao ni ‘vilaza’ kabisa, huwa tunawagawanya katika makundi kulingana na uelewa wao, wenye uelewa wa kwanza, wa kati na wa mwisho. Na mwisho na tunawafundisha kulingana na ‘speed’ (kasi) ya uelewa wao na wanajikuta wanafanya vizuri.

“Lakini kwa sababu sisi tunakuwa na wanafunzi ambao ni wagumu sana, inapoonekana wakatokea wachache hawawezi kabisa huwa tunashauriana na wazazi wao, kuwapeleka Veta ili kule wanapokuwa wanaendelea kujifunza, wengine wanafanya vizuri hadi wanafika vyuo vikuu, hatuwaachi kama ilivyo katika shule za serikali na vyuo vya serikali, haya maneno mengine yanayozungumzwa ni ya kisiasa tu."

HALI ILIVYO

Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika hivi karibuni katika baadhi ya mikoa, ulibaini baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wamekuwa na utaratibu wa kuchuja wanafunzi kila mwaka kwa lengo la kupata wenye uwezo mkubwa darasani.

Ilibainika kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanywa kwa nia ya kuwa na wanafunzi wenye uwezo mkubwa ili shule hizo zifanye vizuri katika mitihani ya taifa, hivyo kuvutia wazazi wengi zaidi kupeleka watoto wao.

Gazeti hili lilibaini kuwa, baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikiendesha utaratibu huo kipindi cha mitihani ya mwishoni mwa mwaka kwa kuwafukuza, kuwakaririsha darasa au kuwahamishia shule nyingine wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango kinachowekwa na shule husika kwenye mitihani ya kufunga mwaka.

Nipashe pia ilibaini baadhi ya shule hizo zimekuwa na utaratibu wa kuwachuja kwa kuwasajili kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) kwenye mitihani ya taifa wanafunzi wake wanaoshindwa kiwango kilichowekwa wanapofanya mitihani ya shule husika.

MTOTO WA PROFESA AKACHA KULA

Akizungumzia suala hilo katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada ya Kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Allen Mushi, alisema haungi mkono utaratibu wa baadhi ya shule binafsi kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango cha alama zilizojiwekea.

Alisema: "Ni makosa kumfukuza shule mwanafunzi aliyekuwa amedahiliwa, anasoma halafu unamsitishia, unamwambia nenda katafute shule nyingine.

"Na ni kweli wana tabia hiyo. “Nina kijana wangu yuko ‘Form One’ (Kidato cha Kwanza) anasoma shule ... (anataja eneo ilipo shule hiyo), yaani anasoma kupindukia. Nilikuwa na wasiwasi hata akija likizo hawezi kula vizuri, anasoma tu."

Alisema kuwa katika shule hiyo ya jijini Dar es Salaam anayosoma mtoto wake, wameambiwa ni lazima awe na wastani wa kuanzia alama 50 katika mitihani ya shule ili aruhusiwe kuingia kidato kinachofuata, vinginevyo wakatafute shule nyingine.

"Katika utaratibu wa elimu, siyo sahihi kufanya hivyo, wewe kama wanafunzi wameshindwa, wewe siyo ndiyo mwalimu, ndiyo kazi yako ya kufanya wanafunzi waelewe," alisema na kufafanua zaidi:

“Sasa ukiwa unafanya hivyo, mwisho wa siku utakuwa unafelisha darasa zima na kujitamba kwamba unafaulisha kwa sababu umefukuza wengi na kubaki na wazuri wachache. Sasa hiyo ni biashara, siyo elimu tena. Wewe kama ni mwalimu, unatakiwa kufundisha wanafunzi wote.

“Kwa hiyo, wanasema shule za ‘private’ (binafsi) zinafaulisha wanafunzi wote, kumbe wengine mliowachuja. Mimi binafsi sikubaliani na hali hiyo kabisa."

Alisema ni muhimu wizara yenye dhamana ya elimu nchini iweke masharti kwamba ukishadahili wanafunzi, wasiondolewe shuleni kwa utaratibu wa viwango vya ufaulu katika mitihani ya shule husika isipokuwa kwa sababu za tabia mbaya na zisizofaa kwa mwanafunzi kwa mujibu wa sheria za nchi.

MAKUNDI YA UELEWA

Msomi huyo alisema wanafunzi wamegawanyika katika madaraja mawili kiuelewa darasani, la kwanza likiwa la wenye uelewa wa haraka (fast learners) na jingine likiwa la wenye uelewa hafifu (‘slow learners).

"Wote hao wanapaswa wazingatiwe katika elimu. Sasa hawa (shule binafsi) wenyewe wanaangalia 'fast learners' tu. Ni vema wote wakachukuliwa katika vigezo sawa, siyo unawachuja wengine halafu unasema unafaulisha wote," alisema Prof. Mushi.

BIASHARA

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba, akizungumza na Nipashe jana kuhusu changamoto hiyo, alisema si vyema kumfukuza, kumkaririsha darasa au kumhamisha mwanafunzi aliyefanya vibaya katika mitihani ya shule.

"Mtihani wa Kidato cha Pili ni mchujo sahihi tu. Shule binafsi wanakosea. Ufundishaji wa kawaida huwezi kuwa na wanafunzi wanaopata daraja la kwanza na la pili tu," alisema.

"Hao shule binafsi kuna muda wanateleza kidogo, kwa sababu hakuna mwanafunzi asiyefundishika labda kwa sababu wao wanataka suala la biashara. Ni kuonea wanafunzi, bahati mbaya akishaanza shule ya 'private' (binafsi) kidato cha kwanza, hawezi kurudi kwenye mfumo wa serikali, kwa hiyo wanafunzi wanahangaika," alisema zaidi Mukoba.

Polisi Yanasa 200 Kwa Ujambazi Dar



JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 200 wanaohusishwa na makosa mbalimbali.

Wanne kati ya hao, wanatuhumiwa kukutwa na gari lililoibwa hivi karibuni katika eneo la ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA) zilizopo Manispaa ya Ilala.

Mkuu wa Operesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alitaja watu hao wanne wanaotuhumiwa kukutwa na gari hilo kuwa ni Leonard Said, Omary Said, Shomaly Kilobo na Adam Unemba.

Alisema katika uchunguzi wa awali, watuhumiwa wote wamekiri kuhusika katika wizi wa gari hilo, aina ya Toyota Spacio lenye namba za usajili T 398 CAE, boksi la chuma la kutunzia fedha na televisheni ya ukubwa wa inchi 32.

Alisema Desemba 5, mwaka huu alipokea taarifa kutoka kwa Mhasibu Mkuu wa TIRA, Egnance Edward (53) kuwa wamekuta ofisi za mamlaka hiyo, zimevunjwa na kuibwa baadhi ya vifaa ikiwemo gari hilo.


KWANINI Wachagga Hupenda Kwenda Kwao Mwishoni Mwa Mwaka?



Nimeamua kuandika kipande cha waraka huu kutokana na kuwepo kwa dhana nyingi potofu juu ya wachagga kwenda kwao kipindi cha mwisho wa mwaka, maarufu kama "kwenda kuhesabiwa".
Je ni kweli wachagga huenda kuhesabiwa? Jibu ni Hapana.. si kweli. Wachagga hawaendi kuhesabiwa.
SWALI; Sasa kama hawaendi kuhesabiwa neno "kuhesabiwa" limetoka wapi na kwanini litumike kwao tu sio kwa Wasukuma, Wamasai, Wayao au Wamakonde?

JIBU; Neno "kuhesabiwa" limetoholewa kutoka neno la Kiebrania "מִפקָד אוֹכלוּסִין" linalomaanisha Wana wa Israel kurudi kwao kwa ajili ya kuhesabiwa.

Mara nyingi Waisrael walikua wanarudi kipindi cha mwisho wa mwaka wa Kiyahudi ktk mwezi uitwao "Adar Beit" ambao kwa mujibu wa Kalenda ya Kiyahudi huo ndio mwezi wa mwisho wa mwaka. Na hukaa huko hadi mwezi wa kwanza wa mwaka ambao kwa kiyahudi huitwa "Nissan".
Utamaduni huu ulitumika ktk Israel ya zamani (Ancient Jews) japo kwa sasa haupo tena. Katika kipindi hiki Waisrael walikua wakikutana nyumbani na kupanga mipango ya maendeleo pamoja na kuhesabiwa ili kujua idadi yao kutokana na kutawanyika katika mataifa mengi duniani.
Tangu enzi za Musa miaka zaidi ya 4,000 kabla ya Kristo; Waisrael walikua na utamaduni wa kurudi kwao kuhesabiwa.

Katika kitabu cha 1 Nyakati 23:2-3 Biblia inasema "Akawakusanya wakuu wote wa Israeli, pamoja na makuhani na Walawi. Nao wakahesabiwa Walawi wenye miaka thelathini na zaidi; na jumla yao kwa vichwa, mtu kwa mtu, ikapata thelathini na nane elfu."

Huu ni udhibitisho wa kuhesabiwa kwa Wana wa Israel zamani hizo. Lakini pia kitabu cha Hesabu 3:14-15 kinasema "Kisha Bwana akanena na Musa huko katika bara ya Sinai, na kumwambia, Uwahesabu wana wa Lawi kwa kuandama nyumba za baba zao na jamaa zao; kila mtu mume tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi utawahesabu."

Maandiko yanayoeleza juu ya kuhesabiwa kwa wana wa Israel ni mengi na unaweza kuyasoma baadae ktk (Kutoka 12:37, Waamuzi 20:14, 1 Samweli 11:8, Ezra 2:64).
Kwa hiyo kuhesabiwa ni agizo la Mungu na utamaduni huu wa wana wa Israel kurudi kwao kwenda kuhesabiwa ni utamaduni uliokua maagizo ya Mungu mwenyewe (Jehovah).
Sasa je ikiwa Wachagga hawaendi kuhesabiwa iweje wafananishwe na WaIsrael?
Sababu mbili hufanya wachagga kufananishwa na utamaduni huu wa Israel wa kuhesabiwa.
SABABU YA KWANZA ni kitendo cha wachagga kurudi kwao mwishoni mwa mwaka (December) na kukaa huko hadi mwanzoni mwa mwaka mpya (January). Ikumbukwe wana wa Israel nao huenda kwao mwishoni mwa mwaka wa Kiyahudi (Adar Beit) na kurejea mwanzoni mwa mwaka mpya (Nissan). Ufanano huu wa majira hufanya wachagga nao waonekane kuwa wanaenda "kuhesabiwa" kama waIsrael.

SABABU YA PILI ni mtawanyiko wa jamii hizi mbili. Wana wa Israel wametawanyika ktk mataifa mbalimbali duniani. Kutokana na ufinyu wa nchi yao wamejikuta wakisambaa nchi mbalimbali ambapo wanaishi na kufanya kazi huko. Wengine ni wahandisi, madaktari, majemadari wa vita etc. Wana wa Israel wametawanyika mataifa yote ya Ulaya, America na baadhi ya nchi za Asia na Afrika. Pamoja na kutawanyika huku lakini mwisho wa mwaka hukumbuka kurudi kwao.
Kwa upande wa wachagga nao wametawanyika sana ktk mikoa mbalimbali nchini. Mtawanyiko wao unafananishwa na ule wa wana wa Israel kwa sababu mbili. Kwanza eneo lao la makazi (Kilimanjaro) ni dogo na haliwatoshi, sawa na Israel ilivyo ndogo na isivyotosha watu wake. Pili ni "nature" ya mtawanyiko wao. Wachagga kama Waisrael wametawanyika sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi.

Hakuna mkoa au Wilaya yeyote unaweza kwenda nchini ukamkosa Mchagga. Wametapakaa kila kona ya nchi wakifanya shughuli mbalimbali hususani biashara. Mtu mmoja aliwahi kutania kuwa "ukienda eneo la nchi hii ukakosa Mchagga ondoka haraka maana hapafai kuishi".. Hii ina maanisha Wachagga wanaweza kuishi ktk mazingira yoyote na hali yoyote.

Mtawanyiko wa Wachagga ktk maeneo mbalimbali ya nchi hufananishwa na mtawanyiko wa Waisrael ktk maeneo mbalimbali ya dunia, na hivyo basi kitendo cha Wachagga kurudi kwao mwishoni mwa mwaka hufananishwa na kitendo cha Waisrael kurudi kwao mwishoni mwa mwaka wa kalenda ya kiyahudi. Tofauti ni kuwa Waisrael huenda kuhesabiwa lakini Wachagga hawaendi kuhesabiwa.
KAMA WACHAGGA HAWAHESABIWI, WANAENDA KUFANYA NINI?
Pengine hili ndio swali la msingi ambalo wengi wanajiuliza. Ikiwa wachagga hawaendi kuhesabiwa kama ilivyo kwa waisrael, Je wanaenda kufanya nini?

Ukweli ni kwamba Wachagga wanakwenda kwao kwa sababu mbalimbali. Leo nitaainisha kwa uchache sababu 10 zinazorudisha wachagga kwao kila mwisho wa mwaka. Zipo nyingi zaidi ila kwa kifupi ni kama ifuatavyo;
1. Kuna wanaokwenda kwao kwa ajili ya kuonana na familia zao na kuwaona wapendwa wao na kujumuika nao kwa ajili ya kufurahia sikukuu za mwisho wa Mwaka huhusani "Krismasi" na "Mwaka mpya".

Kwa mfano wazazi wako (baba na mama) au ndugu zako wengine (babu, bibi, kaka, dada, shangazi, wajomba etc) hujawaona kwa kipindi cha mwaka mzima. Mmekuwa mkiwasiliana tu kwa simu. Hivyo basi December huwa ni kipindi kizuri cha kurudi nyumbani na kuwaona na kuwajulia hali.

2. Pia kipindi hiki hutumika kupanga mipango ya maendeleo ya familia kama vile kujenga. Kwa kuwa watoto wote wa familia hukutana kipindi hiki basi huweka mipango ya maendeleo kwa familia yao. Wanaweza kupanga kujenga nyumba kwa ajili ya wazazi wao ambao ni wazee, kuweka umeme, maji etc.
Uchaggani ni mojawapo ya maeneo nchini ambako kuna nyumba nyingi za kisasa vijijini na ni mkoa uliofanikiwa kupiga vita nyumba ya Nyasi tangu mwaka 1996.
Ni jambo la Kawaida kukutana na maghorofa ya kisasa kule "Machame Uswaa, Kibosho Kirima, au Mamba Komakundi".. au ukipita "Uru Mawela, Rombo Mamsera au Kilema Poffo" nyumba zote unazokutana nazo ni self-contzined za kisasa, lakini wanaishi wazee. Watoto wao wapo Shinyanga, Dar, Kigoma, Mwanza etc wanatafuta maisha. Mipango hiyo ya kujenga na kuhudumia wazazi hupangwa msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

3. Msimu huu wa sikukuu hutumika kupatanisha ndugu, jamaa au marafiki waliokosana. Wazee huitwa na kuzungumza na pande zote mbili kisha kuwapatanisha. Mkikubali kuelewana basi huchinjwa mbuzi kama ishara ya furaha ambapo jamii yote hujumuika kwa kula na kunywa.

4. Kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ndio kipindi kizuri ambacho vijana hukitumia kutambulisha wachumba zao nyumbani. Unaweza kuwa unaishi Dar na umepata mchumba wa Morogoro. Lakini ndugu zako wametawanyika. Wengine wapo Tabora, wengine Mwanza, wengine Mbeya. Huwezi kupita na mchumba wako kote huko kumtambulisha. Kwahiyo "option" nzuri ni kusubiri msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo ndugu zako wote watakuwepo nyumbani ndipo umpeleke mchumba wako kumtambulisha, na kupanga mipango ya ndoa.

5. Kuwaleta watoto wafahamu ndugu zao na wafahamike nyumbani. Unaweza kuwa unaishi Dar na familia lakini ndugu zako wanaishi na familia zao maeneo mengine ya nchi, watoto wenu hawafahamiani maana hawajawahi kuonana. Hivyo mkikutana nyumbani msimu wa sikukuu ni kipindi kizuri cha watoto wenu kufahamiana na kufahamu asili yao.
Pia ikiwa umejaliwa mtoto ukiwa huko unakofanyia shughuli zako lakini wazazi wako hawajamuona mjukuu wao, hiki ni kipindi kizuri cha kuwapelekea wazazi wako mjukuu wao wamuone na kumpa baraka.

6. Kushiriki shughuli za kijamii (charity work). Wachagga wengi ni waumini wazuri sana wa dini iwe ukristo au uislamu. Hivyo kipindi cha msimu wa sikukuu hutenga muda wa kutembelea wagonjwa, Yatima na Wasiojiweza na kuwapa misaada mbalimbali. Kwa wale Wakristo huita "sadaka ya Epifania".

7. Kipindi hiki hutumika pia kufanya usafi na kurekebisha maeneo waliyopumzika wapendwa wetu (makaburi). Wachagga kama ilivyo binadamu wengine hutenga maeneo maalumu ya kuzikia ndugu zao; na mara nyingi kila familia ina eneo lake.

Kwa hiyo ikiwa kuna ndugu amefariki na akazikwa basi msimu huu huwa ni kipindi kizuri cha kujengea makaburi kama kumbukumbu ya sehemu walipopumzika wenzetu.
Bahati mbaya wapo watu wanaohusisha utamaduni huu na matambiko. Kwanza ieleweke kujengea makaburi si dhambi na si matambiko. Hata Yakobo alipofia kule Misri alipoenda kwa mwanae Yusufu alizikwa kwenye Kaburi lililojengewa (Matendo 7:15-16). Hivyo basi ni vizuri ikaeleweka kuwa kujengea makaburi si dhambi.

Na mara nyingi uchaggani kabla ya kujengea Kaburi kiongozi wa dini huitwa na kufanya sala, kabla ya shughuli ya ujenzi haijaanza. Kwahiyo hakuna nafasi ya matambiko.
Ikiwa kuna mchagga anafanya matambiko wakati wa kujengea makaburi ichukuliwe kuwa ni tabia ya mtu binafsi na isihuhishwe wachagga wote. Kwani wapo watu wa makabila mengine hufanya matambiko pia lakini huwezi kusema jamii yote hutambika.
8. Msimu huu wa sikukuu ni kipindi kizuri ambacho wachagga hukitumia kupanga na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii yao kama vile mashule, hospitali, Maji, barabara n.k
Kwa mfano zipo barabara nyingi ambazo zimejengwa kwa nguvu ya wananchi wenyewe kwa kuamua kujichangisha bila kusubiri serikali ifanye. Barabara ya Uru Kusini ni mojawapo. Mipango hii hupangwa msimu huu wa sikukuu.

9. Msimu huu hutumika kwa ajili ya mapumziko ya familia baada ya mahangaiko ya mwaka mzima. Ni wakati wa familia kutulia pamoja kutafakari mipango ya mwaka uliopita na kuweka mipango mipya ya mwaka unaofuata.
Ndugu na jamaa hukutana pamoja na kufurahia sikukuu za "Krismasi" na "mwaka mpya" kwa kula na kunywa hasa vyakula vya asili kama "kisusio, faya, supu ya mbuzi iliyopikwa kiasili kwa kuchanganywa na majani aina ya "mahombo" na vyakula vingine bila kusahau kinywaji aina ya mbege.

10. Kipindi hiki hutumiwa kujenga na kukarabati nyumba za ibada. Ni wazi kuwa Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo ambayo kuna nyumba nzuri na za kisasa za Ibada.
Kanisa kubwa na la kisasa kama la KKKT Old-Moshi Rau, au La RC Kristu Mfalme, Au TAG Kilimanjaro Revival, au Msikiti wa kisasa kama wa Riadha, ni nadra kuvipata mahali pengine. Au Kanisa la kale kama la KKKT Old-Moshi Kidia lililojengwa mwaka 1843 utalipata wapi kwingine?
Mipango ya ujenzi wa nyumba hizi za ibada za kisasa na kukarabati zile za zamani hufanywa msimu huu wa sikukuu.

Pia wachagga wengi hupenda kwenda kwao kwa kuwa ibada zote ktk msimu huu huongozwa kwa kichagga. Yani kuanzia usomaji wa misa, mahubiri hadi nyimbo huimbwa kwa kichagga, wakati huo nyumba za ibada zimepambwa kwa mapambo ya asili kama "Makurera, makangachi, migomba imechimbiwa vichumini (njia za kwenda nyumbani)" etc.

Hii huongeza nakshi na kufanya mtu ajisikie kupungukiwa kitu ikiwa hatakuwepo Nyumbani msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

NB: Utamaduni huu wa Wachagga ni mzuri sana, na kuna mengi jamii nyingine zinaweza kujifunza kupitia Wachagga kama ambavyo wachagga wanaweza kujifunza kupitia jamii nyingine.
Tuukatae uzungu, tujivunie vya kwetu. Jivunie usukuma wako, jivunie Usambaa wako, jivunie Unyakyusa wako, jivunie Umasai wako, Jivunie Ungoni wako, najivunia Uchagga wangu. SI KOSA kujivunia kabila lako lakini NI KOSA kutumia kabila lako kumbagua mtu wa kabila jingine.

Henry Kilewo


TATU Bora Mchezaji Bora Afrika Zatoka



Mshambuliaji raia wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang, mshambuliaji na winga wa Algeria Riyad Mahrez na winga wa Senegal  Sadio Mané wameingia kwenye orodha ya wachezaji wattau bora wa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika.

Wachezaji hao watatu wamefika hatua hiyo baada ya kupigiwa kura na makocha na wakurugenzi wa ufundi wa vyama vya soka vilivyokuwa chini ya  CAF, kamati za vyombo vya habari, kamati za soka na ufundi na wataalamu wa habari. Mohamed Salah na Slimani hawajafanikiwa kuingia katika hatua hii.

Kwa mchezaji bora wa Afrika kwa ligi za ndani, golikipa wa Uganda Dennis Onyango na Mzimbabwe Khama Billiat na mchezaji wa Zambia kiungo Rainford Kalaba wameingia.

TWashindi watatangazwa kwenye tuz hizo maarufu kama Glo-CAF Awards Gala siku ya Alhamis, 5 January 2017 jijini Abuja, Nigeria.

 

Mchezaji bora wa Afrika

Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon & Borussia Dortmund)

Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City)

DIAMOND na Timu yake Kuchoma Gari Moto Jukwaani Kesho Wasafi Beach Party



Kama Kichwa cha habari kinavyojieleza Meneja wa Diamond Sallam Sk Mendez Akihojiwa na XXL leo Live pale mlimani City amesema wanapanga kupandisha gari Jukwaani na kulipiga kiberiti live watu wakishuhudia siku ya kesho Kwenye Party ya Wasafi ...

Amedai stunt kama hizo zinasaidia kufanya mziki wetu uendelee kuwa gumzo Afrika na kukua zaidi.....

SERIKALI yapiga Marufuku Kuagiza Nyama ya Kuku Kutoka nje ya Nchi



Serikali imepiga marufuku kuagiza na kuingiza nyama za kuku waliochinjwa kutoka nje ya nchi ili kulinda afya za walaji wa bidhaa hiyo ya nyama nchini.

Katazo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Tate Ole Nasha kwenye mahojiano maalum na EATV ilipotaka kupata ufafanuzi wa serikali kuwa inahakikisha vipi nyama na vitoweo kutoka nje ya nchi zinaingizwa nchini zikiwa na ubora unaokidhi viwango vya afya kwa walaji.

Ole Nasha amesema hairuhusiwi kuagiza wala kuuza kuku waliochinjwa kutoka nje ya nchi kwakuwa kwa sasa nchi inajitosheleza na inajitegemea kwa kiwango kikubwa cha nyama.

Amewataka wafugaji na wafanyabiashara kutumia fursa za kuzalisha nyama kwa tija na ubora zaidi ili nchi ianze kuuza vitoweo vya nyama hasa kuku nje ya nchi.

Ameongeza kuwa tayari serikali inaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa viongozi wanaoshirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza nyama hizo za kuku wa nje nchini.

DEREVA Bodaboda Akatwa Sikio Kwa Tuhuma ya Kufumaniwa na Mke wa Dereva Teksi



Dereva bodaboda wa Mji Mdogo wa Qatesh wilayani Hanang’ Mkoa wa Manyara, amekatwa sikio kwa kisu kwa tuhuma za kufumaniwa akiwa na mke wa dereva wa teksi.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi, Francis Massawe alisema tukio hilo lilitokea Desemba 21 saa 6:10 usiku kwenye Kitongoji cha Qendangonyi, Kata ya Ganana wilayani Hanang’.

Kamanda Massawe alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi na majeruhi amepata kilema cha maisha baada ya sikio kutolewa.

Alisema wanamshikilia dereva teksi kwa uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kumfikisha mahakamani.

Source: Mwananchi

Thursday, December 22, 2016

RAIS Magufuli Akataa Shule Kuitwa Jina Lake



Rais John Magufuli amekataa shule ya msingi iliyojengwa hivi karibuni eneo la Bunju, Wilaya ya Kinondoni kuitwa kwa jina lake badala yake ameagiza iitwe kwa jina la Mkuu wa wilaya hiyo, Ally Hapi.

Taarifa ya badiliko la jina haikutolewa na Idara ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kama ilivyozoeleka bali na mkuu wa wilaya hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi kwa uongozi wa shule hiyo.

“Shule hii imejengwa kwa fedha zilizopatikana baada ya Serikali Kuu kubana matumizi. Tukaamua iitwe John Magufuli lakini yeye akatoa agizo shule ipewe jina la mkuu wa wilaya sina budi kukubaliana na hilo,” alisema Hapi.

Shule hiyo mpya iliyopo Bunju jijini imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Bunju A ambayo ilikuwa na wanafunzi 3,224.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo mpya, Ali Mwakapalila alisema ingawa inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9 mwakani inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Hakuna umeme wala maji, hii inaweza kuleta madhara kwa wanafunzi hasa linapokuja suala la matumizi ya vyoo,” alisema.

Baada ya hafla hiyo, Hapi alikwenda kwenye kiwanda cha saruji cha Twiga Cement ambako alipokea msaada wa mifuko 600 ya saruji kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa madarasa na majengo mengine.

Akipokea msaada huo, Hapi alisema msaada kutoka Twiga Cement unaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoipa sekta ya elimu kipaumbele ili kuhakikisha inatolewa katika mazingira bora.

“Msaada huu umekuja muda muafaka. Tumeshajenga shule ila tunataka kuongeza madarasa, maabara, ofisi ya elimu na kuzungushia uzio ili watoto wawe katika mazingira salama. Lengo ni kuifanya shule hii iwe ya kisasa na itakuwa mfano kwa shule zote za Wilaya ya Kinondoni,” alieleza.

Pia, Hapi alisema wilaya hiyo ipo kwenye mipango ya kujenga maktaba ya kisasa kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya saruji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twiga Cement, Alfonso Velez alisema kuchangia katika shughuli za kijamii ni moja ya mambo ambayo wamekuwa wakiyapa kipaumbele zaidi.

“Kushiriki shughuli za maendeleo katika jamii ni jambo ambalo tunalipenda zaidi. Yalipo maendeleo Twiga Cement ipo pia,” alisema Velez. VIDEO

Tuesday, December 20, 2016

KIWANGO cha Pesa Kesi za Mafisadi Kushushwa Chini ili Kuwabana Wengi



WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema serikali inatarajia kujadili kushusha kiwango cha fedha kinachohusika katika makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kwenye mahakama ya mafisadi ili kukomesha vitendo vya rushwa.

Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

“Nimeulizwa sana na waandishi wa habari tangu Julai hadi sasa walitegemea kungekuwa na kesi nyingi lakini kuna kesi moja katika Mahakama ya Mafisadi tumekuja kubaini kwamba uchache wa kesi ndiyo mafanikio makubwa ya hatua ya kisheria tuliyochukua,”amesema.

Aliongeza kwa sasa waliozoea kupora mabilioni wamerudi nyuma ambapo wezi hao wameonekana wakiiba fedha chini ya Sh bilioni moja iliyopo kisheria hivyo wanategemea kujadili sheria hiyo ili iwalenge hata wanaochukua kiasi kidogo.

“Sisi kama serikali tukiona wizi sasa umenza kupungua na kuenea katika viwango vya Sh milioni 400, 500, 700 tumeanza kujadiliana kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha ili tuweze kukomesha kabisa udokozi, ubadhilifu, wizi wa fedha au mali ya umma,”alisema.

Aidha alifafanua uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kutafuta vijana wanaojua sheria ili kusaidia wananchi kabla ya kwenda mahakamani ni mzuri.

Aliongeza kuwa tayari wamepeleka mswada wa msaada wa kisheria ambao utasaidia wananchi hasa wa vijijini na wanawake ambao ndiyo wanaumizwa na desturi zilizopitwa na muda ili kuwasaidia kupata haki na itakuwa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima wapatao 4,900.

Makonda alisema wamejadili utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati kwani kuna changamoto ya watu kuwa wengi na kuchelewa kupata haki zao.

Alisema kwa kuona adha hiyo mkoa huo kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya watajenga Mahakama za Mwanzo 20 ili kuongeza kasi za utoaji na upatikanaji wa haki kwa wananchi endapo wanapopelekwa vituo vya polisi
Powered by Blogger.