HAKUNA aliyeaibika wakati akijaribu kufanya jambo kwa faida yake. Siku zote kufanya jaribio ni mwanzo wa kuelekea kwenye ufanisi mzuri wa jambo husika.
Rafiki zangu, ni vema nawe ukajiwekea utaratibu wa kujaribu kufanya mambo ambayo unadhani huyawezi, lakini yakileta matokeo chanya yatakuwa na faida kubwa kwako.
Kujaribu kupo katika mambo mengine mengi ya kawaida – ya kibinadamu. Katika mambo mbalimbali ya kila siku. Ukianza na kupata matokeo mazuri, unakuwa mshindi na bila shaka unakuwa umefanikiwa.
Hali ni tofauti katika suala la mapenzi, huku hakuna kujaribu – ni kuamua tu! Hata hivyo, wakati unaamua mambo yako yanayohusu mapenzi ni lazima kichwani mwako utambue kuwa unafanya kitu kwa ajili yako na mtu mwingine (mpenzi wako).
Hapo ndipo kazi inapokuja. Kwa maneno mengine, wakati ukijifikiria wewe katika ulimwengu wa mapenzi, unatakiwa pia kumfikiria mpenzi wako.
Kwa bahati mbaya, katika eneo hili, wanaume wengi huwa hawafikirii sana namna ya kuwafurahisha wenzi wao. Wanahisi ni suala linalowahusu wanawake pekee. Ni kosa.
Kama mwanaume lazima upate wakati wa kujua unatakiwa kufanya nini kwa ajili ya kulifanya penzi lako lizidi kuchanua.
Hapa katika Love Moment, nimekuandalia mambo ambayo wanawake wengi wanavutiwa zaidi kutoka kwa wanaume.
Je, wewe ukoje? Una sifa hizo? Hebu twende pamoja katika mada hii ambayo bila shaka itakutoa matongotongo.
USAFI BINAFSI
Asilimia kubwa ya wanawake wanapenda sana usafi. Ni aghalabu sana kukutana na mwanamke asiyejipenda. Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya nyumba au ua la nyumba! Ni kwa sababu ya hulka yao ya kupenda sana usafi.
Mwanamke anavutiwa sana na mwanaume mtanashati. Usafi wako unamfanya ajiamini kuwa na wewe. Hata nyumbani kwako, lazima uishi katika nyumba safi. Hata anapokuja kukutembelea, anakuta mazingira masafi kuanzia sebuleni hadi chumbani.
Anapokukuta katika hali ya usafi, inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo alipokukuta na kuendelea mbele.
KUJIAMINI
Mwanamke anajisikia salama zaidi akiwa na mwanaume ambaye anajiamini – mwenye uwezo wa kutetea hoja zake na kujieleza sawia. Siyo anayebabaika.
Suala la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni kubwa kuliko hata kumnunulia manukato mapya. Mathalani unakuwa naye katika mtoko, angependa kukuona ukiwa katika hali halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa na mwenye kutoa maamuzi yasiyoyumba.
Wakati mwingine, mwanamke anaweza kukupima hata katika jambo ambalo amekosea yeye, ataangalia unavyotoa maamuzi yako, lakini pia atafuatilia kuona kama utakuwa mwepesi wa kuyabadilisha.
Anataka kuona msimamo wako muda wote. Mwenye kujiamini na mawazo yasiyo na matege wala makengeza!
KUJITETEA
Kipengele hiki hakina tofauti kubwa sana na kilichopita, lakini hapa ni kwenye upande wa kujitetea zaidi. Wakati unapodai haki yako mbele ya mwanamke wako, suala la kujitetea linapewa nafasi kubwa sana.
Wanawake hawapendi kuwa na wanaume ambao wapo tayari kuonewa. Wanataka wenye uwezo wa kusimama kidete kuona haki zao hazichukuliwi kirahisi.
Hili si suala la kutetea tu haki yako pekee kama mwanaume, bali inapobidi kusimamia haki ya mwanamke wako. Nisieleweke vibaya katika hili, lakini mwanaume imara ni yule ambaye ana nguvu – anafanya mazoezi na ambaye yupo tayari kwa lolote!
Inapowezekana, uwe na uwezo wa ‘kuzichapa’ ikiwa mtakutana na vibaka au watu wabaya wenye lengo wa kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru mpenzi wako.
Mwanaume aliye ‘fiti’ ni chaguo la wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu hana nafasi.
KUJALI
Wanawake wanapenda sana wanaume wanaojali. Wanawaona wao ni kila kitu na wanaotoa kipaumbele kwao. Kama huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali mpenzi wako kwa kila hali.
Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa sana ya kuendelea kudumu katika uhusiano hai.
UKARIBU
Kati ya vitu vinavyowapa mshawasha mkubwa wanawake ni pamoja na kusogezwa karibu. Hapa ni kuwa naye katika mambo mengi unayoyafanya kila siku.
Ni vizuri kuwasiliana naye mchana, ukitaka kujua aina ya chakula alichokula siku hiyo au ikiwezekana mchagulie. Ni mambo madogo sana lakini yanayoongeza nakshi katika mapenzi.
Yapo mengi sana ambayo kwa kuyafanya utakuwa umemsogeza mpenzi wako karibu yako. Hebu tumia ubunifu wako ili uweze kuteka hisia za mwenzi wako kisawasawa
0 comments:
Post a Comment