WAMILIKI wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali wameiomba Serikali kufuta mfumo wa GPA unaotumiwa na Baraza la Mitihani (Necta) kupanga madaraja ya mitihani ya sekondari, kwa maelezo kuwa haufai kwa kuwa unahalalisha watahiniwa waliofeli waonekane wamefaulu.
Akizungumza jana Dar es Salaam kuhusu matokeo ya kidato cha pili ambayo yametangazwa na Necta hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alisema matokeo hayo hayaeleweki kwani wameshuhudia baadhi ya wanafunzi wanaoonekana kufanya vizuri chini ya mfumo wa GPA wakati katika mfumo wa madaraja (division) wanaonekana wamefanya vibaya.
Kwa hali hiyo, Nkonya amemwomba Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kufuta mfumo huo hadi pale Necta itakapokuwa tayari kujibu maswali kadhaa ya wadau wa elimu ambao wanaona mfumo huo hauna tija katika kuboresha elimu.
Baadhi ya hoja ambazo zilihojiwa na Nkonya ni kwamba kulikuwa na kasoro gani katika mfumo wa madaraja mpaka ukaja huo wa GPA na akataka kujua ni nani alilalamikia mfumo wa division mpaka ukaondolewa? Alihoji kabla ya mfumo huo kuletwa, ni wadau wapi walishirikishwa?
Alisema TAMONGSCO ilipata taarifa za kuwepo kwa mfumo huo wa GPA kupitia vyombo vya habari na hawakushiriki katika ngazi yoyote ya mijadala ya kisera kama sheria inavyoelekeza.
Katibu Mkuu huyo wa TAMONGSCO alihoji, “Je, alama za chini za gredi D, C,B na A zilibaki kama zilivyokuwa wakati wa mfumo wa division au kuongeza gredi E na B+ ilikuwa mbinu ya kushusha alama za ufaulu na matumizi ya GPA yakaanzishwa kwa lengo la kuficha ukweli kuwa viwango vimeshushwa kwa kiasi kikubwa??
Nkonya pia alihoji mfumo huo una faida zipi na unasaidiaje katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza wanakuwa na ujuzi stahiki utakaowawezesha kuhimili changamoto za soko la ajira na utandawazi?
“Kwa hali hii bado tunaishauri Serikali isitishe matumizi ya mfumo wa GPA hadi pale hoja zetu zitakapopatiwa ufumbuzi,”alisema Nkonya.
0 comments:
Post a Comment