Serikali imesema kuwa kati ya walimu zaidi ya 8,000 wa Sayansi na Hisabati waliotajwa kuhitaji ajira serikalini, ni walimu 2100 pekee waliotuma maombi, ikimaanisha kuwa kuna walimu zaidi ya 5,000 ambao hawajulikani waliko.
Takwimu hiyo imetajwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Angela Kairuki wakati akizungumza na watumishi wa umma wanawake katika Manispaa ya Dodoma katika wiki ya maadhimisho ya miaka 40 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kairuki alikuwa akizungumzia suala la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma, na kusisitiza kuwa ifikapo mwezi Machi mwaka huu watumishi wote wa umma ambao watakuwa hawajawasilisha vyeti vyao vya kitaaluma watafukuzwa kazi.
Amebainisha kuwa katika zoezi lililofanywa na mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (Nida) waligundua watumishi wengi hawana vyeti na baadhi yao wanatumia vyeti feki hasa wa kada ya ualimu kwa kuwa wana uhakika wa ajira pindi wanapomaliza vyuo.
"Kulikuwa na taarifa kuwa kuna zaidi ya walimu 8,000 waliokuwa wanatakiwa kuajiriwa lakini baada ya serikali kutangaza nafasi hiyo ni walimu 2,100 tuu ndiyo walioomba nafasi mpaka sasa.
Sasa hapo suala la kujiuliza je hao wengine mpaka sasa wako wapi kama hawana vyeti feki!? Nataka niwaambie kuwa hakuna mwenye cheti feki atakayesalimika kwenye Utumishi wa umma," amesema Kairuki.
Amesema ni bora aonekane ni waziri anayechukiwa na jamii kuliko kulifumbia macho suala la vyeti feki kwa watumishi wa umma.
"Tumetoa muda wa kutosha kwa watumishi wa umma kuwasilisha vyeti vyao vya kitaaluma bila shaka walifika mpaka hapa kwenu lakini jambo la kusikitisha ni kwamba mpaka sasa kuna baadhi ya watumishi bado hawajawasilisha," alisema Kairuki.....Vyeti hawajaleta na hata namba ya utambulisho (index number) hawaleta sasa wanataka tuwafanyaje??? Nawamegemea tu siri na mkawaambie na wenzenu itakapofika Machi Mosi hawajawasilisha vyeti vyao tunawafukuza kazi."
Amesema kama serikali itaharakisha zoezi hilo watumishi wa umma wanaostahili watapandishwa vyeo na mishahara yao kwa kuwa zoezi hilo limesitishwa kutokana na uhakiki wa vyeti.
0 comments:
Post a Comment