Jumapili mchana, picha za kijana mmoja aliyetambulishwa kama Fredrick Richard zilianza kusambaa mitandaoni, ikidaiwa kuwa amejinyonga, kisa ni mapenzi kwa mwanamke mmoja ambaye alitajwa kwa jina la Rose, kabla ya baadaye jina hilo kurekebishwa na kuwa Mariam.
Tukio hilo lililozua gumzo kubwa lilidaiwa kutokea huko Korogwe mkoani Tanga, ikidaiwa kuwa marehemu alichukua uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa mpenzi wake wa kike, ambaye anadaiwa kuitwa Mariam, aliamua kumuacha na kuolewa na mwanaume mwingine, ambaye alitajwa kuwa anaitwa Robert.
Katika ujumbe uliodaiwa kuandikwa na marehemu huyo, alidai kuwa amechukua uamuzi wa kujitoa roho kufuatia mpenzi wake huyo kumuacha yeye na kukubali kuolewa na mtu aliyetajwa kuwa ni Robert, licha ya kuwa alipata huduma nyingi za thamani kutoka kwa marehemu.
Aidha, ujumbe huo ulimtaja Robert kuwa siyo tu ni rafiki wa marehemu, bali ni bosi wake, hivyo aliamua kutumia cheo chake kama fimbo ya kumchapia. Sambamba na madai hayo, kulikuwepo na picha zilizotajwa kuwa ndizo za mwanamke anayedaiwa kumkoroga Fredrick, akionekana mrembo hasa, pia za Robert.
Kama ilivyo ada yake, RISASI MCHANGANYIKO liliamua kuchimba ili kubaini ukweli wa tukio hilo ambalo licha ya kuzua maneno mengi miongoni mwa wachangiaji mitandaoni, pia liliacha simanzi kwa ndugu na jamaa wa wahusika hao.
KAMANDA WA POLISI MKOA WA TANGA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alipatikana kupitia simu yake ya mkononi na baada ya kuulizwa kuhusu tukio hilo, alikiri kutokea wilayani Korogwe.
“Taarifa hizo zimenifikia, tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita, katika mtaa wa Mbezi wilayani Korogwe. Katika chumba chake alichojinyongea, marehemu aliacha ujumbe mfupi uliosomeka;
“Asilaumiwe mtu yeyote, nimeamua kujinyonga mwenyewe kutokana na matendo yangu.”
Hata hivyo sisi tunaendelea kumtafuta mtu aliyeshirikiana naye kufanya hayo matendo kwa sababu hawezi kufanya peke yake,” alisema.
Mariam.
KUHUSU PICHA ZINAZOSAMBAA MITANDAONI?
Alipoulizwa kuhusu kama marehemu ndiye ambaye picha yake ipo katika mitandao ya kijamii, alisema amesikia juu ya jambo hilo, lakini hawezi kuthibitisha kama huyo ndiye aliyejinyonga na kuongeza kuwa polisi hawafahamu chanzo cha tukio hilo.
Chanzo chetu cha kuaminika kililidokeza Risasi Mchanganyiko kuwa mtu anayeitwa Robert yupo na ni kweli ndiye aliyeonekana katika picha akiwa kwenye gari, lakini hahusiani na habari hizo hata kidogo. Chanzo hicho kilitoa namba za simu za kaka wa jamaa huyo aliyefahamika kwa jina la Sheck, ambapo alipopatikana, alifunguka hivi;
“Sisi tuna nyumba kule Korogwe, ambako kaka yake Fredrick (marehemu) alikuwa amepanga. Ninamfahamu huyo kijana kwa sababu alikuwa akija pale mara kwa mara, Robert anayetajwa siyo huyo ambaye picha zake zipo mtandaoni, huyu ni mdogo wangu na haishi Korogwe, yupo hapa Dar na ana mke na familia yake.
“Mara ya mwisho Robert kufika hapa ilikuwa ni Krismas iliyopita na hata huyo Mariam mwenyewe hamfahamu, kilichotokea naona watu wanataka tu kumchafua mdogo wangu kwa kufananisha majina.”
Fredrick, akiwa amembeba mpenzi wake na Mariam, enzi za uhai wake.
UTATA JINA LA MARIAM
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya uhakika wilayani Korogwe, ni kweli kwamba marehemu Fredrick alikuwa akishiriki mapenzi na msichana mwenye jina la Mariam, lakini pia jina hilo ni la dada yake. Baadhi ya majirani wanasema walikuta ujumbe unaodaiwa kuandikwa na Fredrick ukitaka Mariam asihusishwe na kifo chake kwa namna yoyote, hali inayowatia shaka ni yupi aliyelengwa, iwapo ni dada au mpenziwe.
“Sasa inakuwa vigumu kuelewa ni Mariam yupi ambaye anahusika na tukio hili ambaye marehemu alisema asihusishwe. Kama ni dada yake pengine anaufahamu ukweli juu ya kilichotokea, lakini hata kama ni aliyekuwa mpenzi wake, pia hakuna anayejua lolote, kama amechangia katika kifo hicho au la,” kilisema chanzo hicho na kuongeza kuwa mpenzi wa marehemu huyo, ambaye alikuwa akimiliki saluni wilayani hapo ametoweka tokea kutokea kwa tukio hilo.
HUYU HAPA ROBERT, MSOME ANAVYOSEMA
RISASI MCHANGANYIKO liliweza kumfikia Robert ambaye alikiri kuwa hilo ni jina lake na ndiye mwenye picha zinazosambaa mtandaoni, lakini hana uhusiano wowote na tuhuma zinazotolewa, kwani hata mwanamke anayezungumzwa hamfahamu na hata alipoomba picha zake zaidi na kutumiwa, alishindwa kumtambua.
“Mimi siishi Korogwe na wakati tukio la Fredy linatokea mimi nilikuwa njiani kurudi kutoka Kigoma kuja Dar kikazi. Nimedhalilishwa, nimefedheheshwa sana, nimetukanwa, familia yangu imezodolewa, mke wangu kila anapopita ananyooshewa vidole kuwa mumewe nimesababisha kifo cha rafiki yangu.
“Nimesikitika sana na taarifa za uongo zinazoenezwa mitandaoni ila nashukuru ndugu zake marehemu wamenipigia na kunipa pole na kusema kuwa ukweli wao wanaujua kuwa si mimi ambaye nahusika katika tukio hilo.”
MSIKIE MARIAM, DADA WA MAREHEMU
RISASI MCHANGANYIKO lilimpata dada wa marehemu, Mariam ambaye alisema Robert asihusishwe na kifo hicho kwani hakuna ukweli wowote. Wala huyo Robert anayetajwa kuwa alikuwa na cheo kikubwa kumzidi kaka yake pia siyo kweli, kwani hakuwa akifanya kazi zaidi ya kuwa mtu wa mishemishe tu za kawaida.
“Mimi ninachoona ni kuwa mdogo wangu ameuawa. Kuna watu watakuwa wamemuua na ili kuficha ushahidi, ndiyo wakamtundika na kuanza kueneza maneno ya uongo mitandaoni.”
FREDRICK NI NANI?
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Fredrick alikuwa ni ofisa mikopo katika Saccos iliyomilikiwa na familia yao, iitwayo Single Microfinance Company akiwa amezaliwa mwaka 1989 na alizikwa Jumatatu katika Kijiji cha Kongoto, kilichopo Butiama mkoani Mara.
MWENYEKITI SERIKALI YA MTAA
“Ni kweli tukio hilo limetokea ila habari zinazoandikwa kwenye mitandao ya kijamii nyingi zinaongezewa, zinapotosha ukweli, barua inayosambazwa kuwa imeandikwa na marehemu na ile inayodaiwa kuandikwa na Mariam siyo zenyewe, marehemu aliacha kipande kidogo cha karatasi, sijaona mtu ambaye ameshikiliwa na polisi kuhusu tukio hilo ila nadhani wanaendelea na uchunguzi wao,” alisema mwenyekiti huyo, Rajabu Nzige.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment