VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Kaimu Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama, Selemani Mathew na Katibu wa Chadema Kijiji cha Nyangamara ‘A’ mjini Lindi, wamehukumiwa kifungo cha miezi minane jela bila ya faini kutokana kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi katika kijiji hicho wilayani Lindi.
Viongozi hao waliohukumiwa ni kati ya viongozi sita waliokamatwa na kutuhumiwa kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi nchini.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Lindi, Muhini alitoa hukumu hiyo baada ya kusikiliza mashtaka pande zote mbili na kubaini viongozi hao walitenda kosa la kisheria.
Tukio lililotokea Aprili 3, mwaka jana kwa viongozi na wanachama kwa pamoja kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi wilayani Lindi.
Alitaja kifungu cha sheria kilichovunjwa ni Kipengele 74(1) na 75 kinachozungumzia Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachosomeka kwa pamoja na sheria ya Jeshi la Polisi.
Alisema washitakiwa wengine wanne wanaachiwa huru, kwani walibainika hawana hatia. Hao ni Bashiru Rashidi, Hassani Mchilima, Abdallah Mmasikini na Isimael Kupilila.
Akizungumzia hukumu hiyo, Mratibu wa Wanawake wa Chadema Mkoa wa Lindi, Sina Kikuwi alisema mahakama haikutenda haki kwa watuhumiwa hao.
Alisema taarifa walikuwa nayo kwenye vikao hivyo vya ndani havihitaji kibali, bali kutoa taarifa ambazo zilishatolewa katika mamlaka husika.
Selemani Mathew aliwahi kuwa D
iwani wa Vijibweni wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya CCM. Aligombea katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi mwaka juzi, ambapo katika kura za maoni za CCM alishindwa na Nape Nnauye.
Baadaye alihamia Chadema ambako alikuwa mgombea ubunge wa chama hicho, lakini pia alishindwa na Nape ambaye sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
0 comments:
Post a Comment