Ndugu zangu,
Kuna wakati Mama Maria Nyerere alipata kuulizwa swali la kukera kutoka kwa mwandishi kijana.
Mwandishi huyo alimuuliza Mama Maria Nyerere: “Hivi, inakuwaje Mwalimu
ameondoka na kuacha familia yake ikiishi katika hali ya kawaida sana
bila kuwa na mali nyingi wakati tunaona watendaji wa siku hizi wana mali
na wengine wanasomesha watoto wao nje ya nchi?”
Mama Maria Nyerere alimjibu mwandishi yule: “Naona wewe bado ni kijana sana, hukuwepo wakati
ule wa Azimio la Arusha, lakini hiyo si sababu ya wewe kushindwa kufahamu ya nyuma, maana ulitakiwa kusoma.
Wakati wa Mwalimu kulikuwa na Azimio la Arusha na miiko ya viongozi. Na
Mwalimu kama kiongozi, asingeweza kufanya tofauti na yale ambayo
aliyasimamia na aliwataka wenzake katika uongozi wayafuate.”
Ndiyo, katika utaratibu wa sasa, na hasa baada ya kuondokana na kanuni,
miiko na maadili ya uongozi ya enzi za Mwalimu, ni kawaida kukuta
Watendaji wenye miradi ya biashara, mashamba na hata viwanda ambavyo wao
wenyewe ndio wasimamiaji.
Hivi, Waheshimiwa hawa watapata wapi muda wa kusimamia biashara,
mashamba na viwanda vyao kama si kuiba muda wa kuwatumikia wananchi na
hata kutumia rasilimali za umma?
Inahusu swali hili; Ni nani atauzima mshumaa wa Serikali? Hapa kuna kisa nilichopata kusimulia.
Naam, miongoni mwa viongozi waliopata kuongoza dola ya Kiislam, hususan
baada ya Mtume Muhammad (SAW) na baada ya masahaba, ni Amir muumini na
Khalifa Umar bin Abdulaziz.
Wanazuoni wa Kiislamu wanatwambia, kwa utawala wa Khalifa Umar bin
Abdulaziz ulijaa uadilifu. Si kwa viongozi tu, hata kwa raia wake.
Inasemwa kwamba moja ya mafanikio makubwa ya utawala wa Khalifa Umar bin
Abdulaziz, ni kukusanya zakka. Katika Uislamu, zakka ni ibada ya lazima
kwa mwenye nacho kuwapa masikini, yatima, wajane, wasafiri, raia na
wengineo wenye kuhitaji.
Watu walijengewa imani kubwa, kiasi hakuna aliyethubutu kukwepa kutoa
zakka. Hata wale waliopokea zakka walikuwa waadilifu, hawakupokea zakka
mara mbili kama walishapokea kabla. Wote waliostahili kupata zakka ,
walipata zakka. Hakika, zakka zilitolewa zikajaa mabohari.
Siku moja raia mmoja alikwenda kwenye ofisi ya Khalifa Umar bin
Abdulaziz. Wakati wa maongezi yao, Khalifa Umar alikuwa akihangaika
kuupuliza na kuuzima mshumaa mmoja na kuwasha mwingine.
Alikuwa na mishumaa miwili mezani. Kadri mazungumzo yalivyoendelea, Umar
aliendelea kufanya hivyo. Alipuliza mshumaa mmoja ukazimika, kisha
akawasha mwingine.
Jambo hilo lilimstaajabisha sana mgeni wa Khalifa Umar bin Abdulaziz.
Akauliza: "Je; ni kwanini unazima mshumaa huu na kuwasha mwingine, kisha
huo nao unauzima na kuwasha ule wa kwanza?
Khalifa Umar bin Abdulaziz akamjibu: "Mshumaa huu ni wa Serikali, wewe
unaponiuliza habari za Serikali, nauwasha. Lakini naona mara unauliza
habari za familia yangu, ndiyo maana nauzima wa Serikali na kuuwasha
mshumaa wangu mwingine nilioununua kwa pesa za mfukoni mwangu. Nachelea
nisije fanya dhuluma kwa mali ya nchi."
Ndugu zangu,
Bila shaka, hicho ni kisa chenye kutupa mafundisho muhimu
juu ya dhana nzima ya maadili katika utumishi wa umma. Tafakari!
Bila shaka, hicho ni kisa chenye kutupa mafundisho muhimu
juu ya dhana nzima ya maadili katika utumishi wa umma. Tafakari!
Maggid,
Iringa.
Iringa.
0 comments:
Post a Comment