Thursday, November 26, 2015

Safari za ndani za vigogo na siku ya Ukimwi vyafutwa.

Rais Dk. John Magufuli

Wakati safari holela za nje ya nchi zikidhibitiwa, janga lingine limewashukia vigogo baada ya serikali kutangaza 
kufuta safari za ndani kwa ajili ya mikutano na vikao vya kazi.
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ilitangaza jana kuwazuia watendaji wake kutumia fedha za umma kugharimia safari, kukodi kumbi za vikao na mikutano ya kazi kokote nchini kuanzia sasa.
Badala yake, watendaji hao wa serikali wametakiwa kutumia mfumo wa kisasa wa upashanaji habari kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehema) kufanikisha mikutano hiyo.
  
Kwa mantiki hiyo, kuanzia sasa serikali haitaingia tena gharama za kuendesha vikao vya kazi na watendaji wake kwa kuwa hayo yatatafanikishwa kupitia mfumo wa mikutano ya video mtandaoni.
Mkakati huo mpya na endelevu ulitangazwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Florence Temba, alipozungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa serikali imeanza kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
Alisema walengwa wakuu wa vikao kazi ni Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maofisa Utumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kote.
Temba alitaja gharama ambazo serikali haitaingia tena kuwa ni pamoja na kukodi kumbi, usafiri na muda utakaotumika nje ya vituo vya kazi, hivyo Tehama ndiyo itatumika katika kuendesha vikao kazi vinavyowahusu watendaji wake katika utekelezaji wa majukumu kwenye maeneo ya kazi.
"Menejimenti ya Utumishi wa Umma, inasisitiza kuwa Tehama itatumika kuwa chombo muhimu cha kuboresha utendaji serikalini kwa kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za utendaji na kuboresha utoaji huduma kwa wananachi," alisema Temba.
Alisema kuwa mfumo huo wa kuendesha mikutano ya serikali kupitia mfumo wa picha za video, ni salama kwa sababu miundombinu yote itakayotumika imeratibiwa na kukaguliwa na serikali.
Temba alitaja mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa maandalizi na uendeshaji wa mikutano hiyo kuwa ni pamoja na uhakiki wa mfumo kabla ya matumizi, utunzaji na matumizi ya mifumo ya mawasiliano kwa njia ya video kwa kuzingatia mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama.
Akizungumzia mpango huo utakavyotekelezwa, Mkurugenzi wa Tehama, Priscus Kiwango, alisema katika mikoa yote nchini, ni mikoa mitatu tu mipya ndiyo haijaingizwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Hata hivyo, Kiwangp alisema mikoa hiyo itashiriki vikao hivyo kwa kutumia mikoa jirani ambapo gharama zitapungua.
Aliitaja mikoa ambayo haijaingizwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwa ni Geita, Simiyu na Njombe, huku akisisitiza kuwa itaingizwa kwenye utaratibu kadiri serikali inavyoendelea kujipanga.
"Teknolojia hii itawezesha mawasiliano kutoka vituo mbalimbali kuwasiliana kwa njia ya sauti na picha," alifafanua na kongeza kuwa hivyo inawezesha wahusika kuwasiliana moja kwa moja kwa njia ya kielektroniki bila kuhitaji kukutana pamoja," alisema.
Utaratibu wa Tehama nchini umeanza mwaka mmoja uliopita na tayari umefanikisha mikutano takriban 10 kwa njia hiyo.
Lengo kuu ni kupunguza gharama za mikutano na kuna uwezekano pia wa kufanya mkutano unaoweza kutumia kwa saa tano mfululizo huku mikoa minane ikiwa imeunganishwa pamoja.
Agizo hili la serikali limekuja siku chache tangu Rais Dk. John Magufuli, atangaze kusitisha kwa muda safari za nje ya nchi kwa maofisa wa serikali akisema itasaidia kubana matumizi ya serikali.
Katika maelezo yake hivi karibuni, Rais Magufuli alisema serikali imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya safari za nje kwa maofisa wake wa kada mbalimbali na kuisababishia serikali mzigo mkubwa wa gharama.
Aidha, agizo hilo la serikali linakwenda pamoja na sitisho la muda la maofisa wa serikali kwenda kushiriki semina na makongamano nje ya nchi ambapo ameagiza kuwa hivi sasa watoa mada wataalikwa nchini kufundisha badala ya makundi makubwa ya watumishi kwenda nje ya nchi.
Rais Magufuli pia alizuia matumizi ya fedha zaidi ya Sh. milioni 200 zilizochangwa na wahisani mbalimbali kwa ajili ya sherehe za kupongezana wabunge mjini Dodoma na kuelekeza zitumike kununulia vitanda, magodoro, mashuka na vifaa vingine kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.