SERIKALI imewasimamisha kazi watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ambao jana iliamriwa kwamba watahamishiwa mikoani.
Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw.
Robert Nyoni.
Uamuzi huo umetolewa leo (Jumamosi, Novemba 28, 2015), na Waziri Mkuu
Majaliwa Kassim Majaliwa ili kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma
zinazowakabili.
Kama ilivyo kwa wenzao sita waliosimamishwa kazi jana (akiwemo aliyekuwa
Kamishna Mkuu), nao pia hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi hadi
uchunguzi utakapokamilika.
“Kazi ya kuwachunguza ilianza jana ileile na sasa, tumeona hawa watu
wanapaswa kuwa nje ya utumishi ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru
zaidi,” alisema Waziri Mkuu.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Philip
Mpango atekeleze maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi hao.
Jana mchana, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kushtukiza kwenye bandari ya
Dar es Salaam akiwa na nia ya kukagua namna shughuli zinavyoendelea
kwenye bandari hiyo hasa kwenye maeneo ya kupokelea mizigo kutoka nje ya
nchi.
Katika kikao kilichofanyika bandarini hapo na kuhudhuriwa na baadhi ya
viongozi wa Serikali, Waziri Mkuu aliamua kuwasimamisha kazi maafisa
watano na TRA kutokana na ‘upotevu’ wa makontena 349 yenye thamani ya
zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Waziri Mkuu alisema upotevu huo unasababishwa na mchezo unaofanyika
baina ya wafanyabiashara na watumishi wa TRA ambao wanaruhusu makontena
kupita bila kulipiwa ushuru na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
0 comments:
Post a Comment