Saturday, November 19, 2016

Majibu ya Jeshi la Polisi Makao Makuu kuhusu tuhuma za Rushwa dhidi ya Kamanda Sirro



Jeshi la polisi nchini limesema litafanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa dhidi ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro na baadhi ya makamanda wa mikoa akiwemo kamanda wa mkoa wa Kinondoni Susan Kaganda.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, CP Robert Boaz katika makao makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya CP Boaz kwa niaba ya jeshi la polisi imetolewa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hivi karibuni kuwatuhumu makamanda hao kuwa wanasita kuwachukulia hatua watumiaji na wauzaji wa kilevi cha shisha kwa madai kuwa huenda wakawa wamepokea rushwa kutoka kwa wanaojishughulisha na biashara hiyo.

Makonda alitoa tuhuma hizo licha ya yeye ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama katika kanda hiyo kutoa maagizo wahusika kuchukuliwa hatua.

CP Boaz alisema, kuhusu tuhuma ya rushwa suala hilo lina taasisi zake zinazohusika, na kwamba jeshi hilo limepokea tuhuma hizo dhidi ya askari wao kwa hiyo watazichunguza kubaini ukweli.

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.