Uagizaji huo wa nguzo kutoka nje ya nchi, unaelezwa kwenda kinyume na Sera ya Serikali ya maendeleo ya kiuchumi
Moshi. Rais John Magufuli ameombwa kuzuia uagizaji wa nguzo za umeme kutoka Afrika Kusini kunakofanywa na Shirika la Umeme (Tanesco) kupitia wazabuni ili kunusuru mamilioni ya fedha za kigeni.Vyanzo kutoka Tanesco vimedokeza kuwa shirika hilo liko katika hatua ya mwisho kutangaza zabuni ya nguzo 700,000 ambazo, zinaweza kugharimu Dola 115 milioni (sawa na Sh250 bilioni) kwa mwaka 2015-2018.
Sehemu kubwa ya fedha hizo inatarajiwa kutumiwa na kampuni za nje zinazojipanga kuomba zabuni hiyo ili kuagiza nguzo kutoka Afrika Kusini na Kenya kama ilivyokuwa kwa zabuni ya 2013-2015.
Hata hivyo, Mkurugenzi mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alikanusha kuzibeba kampuni za kigeni, bali akasema katika kutafuta wazabuni, wanaongozwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011.
Sheria hiyo ndiyo ambayo Rais Magufuli wakati analihutubia Bunge Novemba 11, aliikosoa kwamba ni mbaya na kuwa Serikali ingepeleka muswada bungeni ili kuifanyia marekebisho.
Mramba alifafanua chini ya sheria hiyo, kuna zabuni za aina mbili, ambazo ni zabuni kwa kampuni za ndani ya nchi (NCB) na zabuni kwa kampuni za kimataifa (ICB).
Mramba aliwataka wanaohoji nguzo kuagizwa nje ya nchi, wasisahau kuna wakati Tanesco ilitangaza zabuni chini ya NCD, lakini wazabuni wa ndani wakashindwa hadi waziri akavunja zabuni hiyo hadharani.
Kuhusu thamani ya zabuni wanayokusudia kuitangaza hivi karibuni, alisema hafahamu jambo hilo na kushangaa inakuwaje wanaohoji wawe wanafahamu thamani ya zabuni wakati bei hupangwa na wazabuni wanapoomba.
Uagizaji huo wa nguzo kutoka nje ya nchi, unaelezwa kwenda kinyume na Sera ya Serikali ya maendeleo ya kiuchumi inayohamasisha matumizi ya bidhaa za ndani.
Baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco, waliozungumza na gazeti hili, walidai hayo ni matumizi mabaya ya fedha za kigeni kwa kuwa Tanzania inao uwezo wa kuzalisha nguzo za kutosha kwa shirika hilo.
Maofisa hao wa Tanesco, waliliambia gazeti hili jana kuwa zabuni iliyopita ya miaka mitatu (2013-2015), ilisababisha asilimia 65 ya nguzo za umeme kuagizwa kutoka Afrika Kusini.
Ni kutokana na msingi huo, wafanyakazi hao wamemwomba Rais Magufuli kuzuia zabuni hiyo ambayo itatangazwa hivi karibuni. “Kwenye hotuba yake Rais alisema hataki samani ziagizwe nje ya nchi, sioni sababu kwanini hata nguzo zitoke nje ya nchi wakati tuna kampuni zinaweza kusambaza kutoka kwenye misitu yetu,” alidai ofisa mmoja wa Tanesco.
Hata hivyo, chanzo kingine kutoka sekta ya nishati ya umeme, kimedokeza kuwa kanuni za manunuzi zimekuwa zikipendelea kampuni za nje na kuziruhusu kuomba zabuni kwa Dola ya Marekani.
Wataalamu wa uchumi wanadai matumizi ya Dola kuagiza bidhaa ambazo zingeweza kupatikana hapa nchini, yanachangia kuporomosha thamani ya shilingi.
“Kuanzia mwaka uliopita shilingi yetu imeporomoka kwa asilimia 23 ya thamani yake kutoka Sh1,765 kwa Dola moja Desemba mwaka jana hadi Sh2,160,” alidokeza mchumi huyo.
Alisema kununuliwa kwa nguzo zinazozalishwa nchini, kungeongeza mapato ya Serikali kutokana na kodi ya ongezeko la thamani, kodi ya mapato na kodi nyingine ambazo hazilipwi na kampuni za nje.
Pia, itaongeza hamasa ya wananchi kuanzisha vitalu vya miti na wawekezaji kutoka nje ambao wataanzisha mashamba ya miti nchini kwa kuwa kutakuwa na soko la uhakika la Tanesco.
Kampuni za ndani zilizoshinda zabuni ya kusambaza nguzo nchini mwaka huo wa 2013-2015 zilikuwa Critical Engineering Solutions Construction Co, Sao Hill Industries Ltd na Mufindi Wood Poles.Kampuni za nje ambazo ni kutoka Afrika Kusini zilizoshinda zabuni hiyo ni Treated Timbers Products, Low’s Treated Timbers (Ptg), Rousant International na Maghilika Timber Ptg Ltd.
Ofisa Habari wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud alisema hakuna ukweli kwamba nguzo za nje ni ghali kuliko za ndani, bali ni fitna za ushindani wa kibiashara za baadhi ya watu wanaokosa zabuni.
Alisema Tanesco inanunua nguzo kulingana na zabuni, ubora na bei, ziwe za ndani au nje lakini wapo wazabuni wa ndani ambao hushinda, lakini wakashindwa kukidhi mahitaji ya Tanesco.
“Kuna kipindi nikiwa pale Tanesco hata waziri wa nishati aliamua kuingilia kazi na kuwakemea wazabuni wa ndani walioshindwa kukidhi mahitaji ya zabuni,” alisema Badra.
Source;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment