Aliyekuwa Kamishina Mkuu, Rished Bade |
Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kubaini ukwepaji kodi mkubwa ulioikosesha serikali kiasi cha shilingi bilioni 80.
Katika kikao na viongozi wa TPA sanjari na viongozi wa TRA, akiwemo aliyekuwa Kamishina Mkuu, Rished Bade, Waziri Majaliwa aliamuru papo hapo, kusimamishwa kazi kwa baadhi ya vigogo wa bandari.
PANGA LILITUA KWA HAWA
Vigogo waliosimamishwa ni pamoja na Bade, Kamishina wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Tiagi Masamaki na Habibu Mponezya wa Kituo cha Huduma kwa Wateja kisha waziri mkuu akamwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu kuhakikisha wote wanakamatwa.
Wengine waliosimamishwa ni Eliachi Mrema (Msimamizi Mkuu wa Bandari Kavu Dar es Salaam), Haruni Mpande (Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) na Hamis Omar, Nsajigwa Mwandegele, Robert Nyoni na Anengisye Mtafya.
AGIZO ZITO
Kabla hajamaliza kikao, Waziri Majaliwa aliagiza kuwa, licha ya watu hao kukamatwa, hati zao za kusafiria kushikiliwa, pia mali zao zichunguzwe ili kubaini kama zinaweza kumilikiwa na mtumishi wa umma kwa kutumia mshahara wake!
RISASI MCHANGANYIKO LAFUKUA
Kufuatia agizo hilo la Waziri Mkuu katika kipindi hiki cha ‘hapa kazi tu’, gazeti hili liliingia mtaani kwa kufanya uchuguzi wa kina ili kubaini utajiri wa vigogo hao na wengine ambao hawajakumbwa na sakata hilo.
Juzi Jumatatu, Risasi Mchanganyiko lilifika Masaki, Mbezi na Tegeta Madale kwenye makazi ya baadhi ya watumishi hao ili kuona mazingira yao.
Ndani ya nyumba ya mtumishi mmoja, Risasi liliona magari matatu ya kifahari aina ya Toyota Land Cruiser ‘VX’, Mercedes Benz na Range Rover achilia mbali Toyota Noah ambayo majirani walisema huwa inakwenda sokoni kufanyia ‘shopping’.
Kwenye nyumba nyingine, ukuta ulikuwa mrefu kiasi cha wapigapicha wetu kushindwa kuona ndani mpaka wakapiga kengere. Lakini majirani walisema si rahisi kufunguliwa kwa siku mbili hizi kwani kumekuwa na ‘ingia toka’ ya watu wa usalama wa taifa.
“Kama hamna namba za simu za mtu yeyote aliye ndani sijui kama mtafunguliwa. Siku mbili hizi, watu wa usalama wa taifa wanaingia na kutoka,” alisema jirani mmoja.
Jirani huyo alisema jumba hilo mmiliki ni mkaaji mwenyewe ambaye ni mtumishi wa TRA na ana nyumba nyingine maeneo ya Mwenge licha ya kumiliki maduka ya nguo Kariakoo, Dar.
Baada ya hapo, gazeti hili lilifunga safari hadi Pugu ambako kuna makazi mengine ya mmoja wa vigogo hao lakini nyumba ilionekana kuwa kimya na kutokuwepo kwa gari hata moja kwenye eneo la maegesho.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Mjumbe wa Nyumba Kumi Mtaa wa Pugu Bombani, Abdallah Shaban alisema huwa kunakuwa na magari mengi kwenye nyumba hiyo, lakini kwa siku mbili zilizopita (Jumamosi na Jumapili) hajayaona.
“Hapa ‘panakuwaga’ na magari mengi sana. Unaweza kusema ni yadi ya kuuza magari, lakini siku mbili hizi sijayaona,” alisema mjumbe huyo.
MAGARI HAYANA KAZI
Mjumbe huyo alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, kutokana na magari kuwa mengi pasipo watumiaji, mara nyingi asubuhi mmiliki huyo humwagiza mtu mmoja kuyawasha na kuunguruma kwa muda kisha kuyazima kwa lengo la kuyapasha moto.
NYUMBA KAMA KIJIJI
Mjumbe huyo alilionesha Risasi Mchanganyiko eneo kubwa la mtumishi huyo ambapo amejenga nyumba za familia zisizopungua 20 sehemu moja (kama kijiji) na moja tu ndiyo imepangishwa.
UCHUNGUZI WA JUMLA
Uchunguzi wa jumla uliofanywa na Risasi Mchanganyiko ulibaini kuwa, watumishi wengi wa TRA na TPA wanamiliki nyumba na magari licha ya kulipwa mshahara wa ngazi ya serikali ambao wasingeweza hata kununulia gari moja la kifahari kama ilivyo sasa.
GPL
0 comments:
Post a Comment