Sunday, December 6, 2015

Kiama Cha Waliotorosha Makontena 2431 Kimekaribia.....Majina Yao Yameshatua Kwa Waziri Mkuu



Baada ya moto kuwawakia watumishi wa Mamlaka ya Mapato wanaotuhumiwa kujihusisha na ukwepaji kodi wa kifisadi kwenye Bandari Kavu (ICDS) na kupelekea wanane kati ya watuhumiwa 37 kufikishwa mahakamani, zamu ya Mamlaka ya Bandari inakaribia, imefahamika.
 

Watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam, waliohusika na kupitisha makontena 2,431 bila kulipiwa kodi wanakaribia kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria baada ya majina ya wahusika kutua mezani kwa Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, kama alivyoagiza.
 

Kuwasilishwa kwa majina hayo katika Ofisi ya Waziri Mkuu Majaliwa, kunafuatia ziara ya kushtukiza katika Bandari hiyo ambapo aligundua kuwapo kwa ufisadi huo.
 

Katika ziara hiyo, Majaliwa alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga kupeleka ofisini kwake majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji huo wa kodi unaokadiriwa kufikia shilingi bilioni 600 ifikapo saa 11 jioni Alhamisi.
 

Jana  Mwandishi wa Habari wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Irene Bwire, alithibitisha  kuwa majina hayo yameshamfikia Waziri Mkuu.
 

“Ninachoweza kukwambia ni kwamba majina yamefika mezani kwake kama alivyoagiza lakini siwezi kukutajia majina ya wahusika... Waziri Mkuu ndiye mwenye mamlaka ya kuyataja hadharani iwapo ataamua kufanya hivyo,” alisema Irene.
 

Kwenye ziara hiyo, Majaliwa alimpa Meneja huyo siku saba kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye mfumo wa ankara na kuwa wa malipo wa kielektroniki.
 

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka, aliuonya uongozi wa Bandari kutofanya ujanja wa kuficha majina ya watu wakubwa waliohusika na upotevu wa makontena 2,431 yaliyotolewa bila kulipiwa ushuru.
 

Mwinjaka alitoa onyo hilo baada ya uongozi huo kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupeleka majina ya watu hao ofisini kwake juzi.
 

“Lazima uongozi wa Bandari ujihakiki kama watu wote waliohusika katika hujuma ile majina yao yamo kwenye orodha iliyopelekwa kwa Waziri Mkuu,” alisema katibu Mkuu huyo. 
“Hata akiwa papa lazima ajulikane na wasiwachukue watu wadogo wadogo peke yao maana itawagharimu.”
 

Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara nyingine ya kushtukiza bandarini katikati ya wiki kwa kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo wa malipo baada ya kupewa taarifa kuna makontena 2,431 yalitolewa bandarini bila kulipiwa ushuru.
Majaliwa, alikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa mizigo unavyofanyika kwa kutumia Scanners.

 

Katika ukaguzi huo, Majaliwa alieleza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na Azam huku watumishi 10 tu wa ngazi za chini ndio wakiwa wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo.
 

Ziara hiyo ilikuwa ya pili bandarini katika kipindi cha siku tano, baada ya ile ya awali kubaini upotevu wa makontena 349 bila kulipiwa ushuru, kitendo kilichosababisha awasimamishe kazi watumishi tisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bandari, huku Rais John Magufuli akimsimamisha kazi kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade.
Mpekuzi blog

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.