Friday, December 18, 2015

Dkt. Kigwangalla atumbua MAJIPU ya watumishi wachelewaji wa Wizara ya Afya

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla amefanya ukaguzi wa kushtukiza katika ofisi za wizara hiyo kwa kusimama getini kuzuia wafanya kazi wote wa wizara ambao walikuwa wamefika ofisini baada ya saa 1:30 asubuhi* muda ambao ndiyo mwisho wa wafanyakazi kuingia ofisini



Awali Dkt. Kigwangalla alifika ofisini saa 1:05 asubuhi huku akiingia ofisini kwa kutembea mwenyewe bila kutumia usafiri wa gari na kwenda moja kwa moja ofisini kwake ambapo alitoka ilipofika saa 1:32 na kwenda kusimama getini na kisha kuwaamrisha askari wa geti la kuingia katika wizara hiyo kulifunga geti hilo na wasiruhusu mtu yeyote kuingia ndani.

“Fungeni geti na kila atakayefika msimruhusu kuingia ndani ninataka kuona wote ambao wanakuja wamechelewa,” alisikika Dkt. Kingwangalla akiwambia askari wa getini.

Baada ya kutoa amri hiyo alimtaka Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Michael John kumpa vitabu vya kusaini kwa vitengo vyote ili aweke mstari wa kuonyesha kuwa muda wa kuingia ofisini umekwisha na akafanya hivyo kwa kuweka mstari kwenye vitabu vya mahudhurio kuwa muda wa kusaini kuingia umeisha.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo Naibu Waziri alizungumza na wanahabari kuwa ameamua kufanya zoezi hilo katika ofisi za wizara kwa kutaka kuona ni jinsi gani watumishi wa ofisi hiyo wamekuwa na mwitikio wa kufanya kazi kwa kasi anayoitaka rais, Dkt. John Pombe 

Magufuli.



Alisema watumishi hao wameajiriwa na serikali ili kufanya kazi lakini wamekuwa wakichelewa kuingia ofisini na yeye kama Naibu Waziri ana wajibu wa kuwasimamia watumishi hao ili wafanye kazi ambayo serikali imewaagiza kufanya.

“Nina wiki moja tangu nimeingia hapa ofisini kuna mambo ambayo nimeyaona hayapo vizuri na sasa naanza na hili ili tujue kuwa* ni kina nani huwa wanachelewa na zoezi hili litakuwa ni endelevu, kama mimi sitasimamia watumishi wa serikali basi sitakuwa na kazi wizarani tunataka watumishi ambao wanakuwa wanafanya kazi kwa kujitoa kwa ajili ya maslahi ya taifa,” alisema Dkt. Kigwangalla.

Aidha Naibu Waziri huyo alimtaka Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kuhakikisha watumishi wote waliochelewa kufika ofisini wanaandika barua ya kutoa maelezo kwanini wanachelewa kufika ofisini na baada ya hapo Mkurugenzi na yeye atoe maelezo kwanini muda wa kutoka watumishi wanakuwa hawasaini kuwa wametoka.



Pia alishauri uongozi wa wizara ufanye mabadiliko ya mfumo wa watumishi kuingia ofisini kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kadi au kidole “Biometric” ili kuwa na taarifa katika mifumo ya mawasiliano kujua wanaochelewa ofisini na wanaowahi kutoka na baada ya hapo uongozi utajadili adhabu za kuwapa watumishi wote ambao wamekuwa wakichelewa kufika na kuwahi kutoka ofisini.



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla akipitia mahudhurio ya watumishi wa wizara kwa siku zilizopita[/SIZE][/FONT]



0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.