Saturday, December 5, 2015

MAGUFULI ATUA TFF


KASI ya utendaji ya Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli imehamia katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuzua tafrani.

Wakitekeleza moja ya maagizo mapya ya Magufuli kukusanya kodi kwa ufasaha na kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi, maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ilala wamezuia akaunti ya TFF ili ilipwe kodi za nyuma.

TRA imezuia akaunti zote za TFF ikitaka ilipwe jumla ya shilingi 1,637,334,000 (Sh bilioni 1.6) ikiwa ni kodi kwa kipindi cha mwaka 2010-13, sehemu kubwa ikiwa ni makato kwenye mishahara (PAYE) ya makocha Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelsen.

Pia imeelezwa, TRA inataka ilipwe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Brazil uliofanyika mwaka 2010.

Hata hivyo, TFF imesema makocha hao wa timu za taifa wamekuwa wakilipwa mishahara na serikali, hivyo wao hawakuwajibika kuwakata kodi.

Pia shirikisho hilo, limesema katika taarifa yake kwamba, mchezo kati ya Tanzania na Brazil ulisimamiwa na kamati maalum ya serikali na fedha zake hazikuingizwa katika akaunti za TFF.

Kutokana na hali hiyo, TFF imesema ziara ya timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 15 (U-15) kwenda Rwanda, Uganda na Kenya imekufa na badala yake timu hiyo itacheza mechi za kirafiki Mwanza na Kigoma.







Itacheza na Burundi mjini Kigoma kwani haina fedha za kwenda nje ya nchi kutokana na TRA kuzuia akaunti hizo za TFF. Shughuli nyingine za soka zitakazohathirika ni;

Kulipwa kwa madeni ya usafiri, chakula na posho za wachezaji wa timu za taifa zilizoshiriki mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018 na Kombe la Chalenji, pia program za soka la wanawake na vijana zitasimama.

Ile michuano ya Kombe la FA nayo haitaweza kufanyika katika hatua ya raundi ya pili, Ligi Daraja la Pili nayo itasimama. Imeelezwa kuwa, TFF haitaweza kulipia vifaa vya michezo ikiwemo mipira kwa ajili ya shule za msingi na vituo vya maendeleo vinatarajiwa kuwasili nchini muda wowote.

Pia kuna hatari kutolipwa kwa mishahara ya wafanyakazi wa TFF, kutolipwa kwa gharama za kambi na karo kwa ajili ya vijana wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 13 walioko Shule ya Alliance Academy ya jijini Mwanza.

Oktoba 2012 na TRA ilichukua Sh 157,407,968 iliyokuwa mgawo wa klabu lakini yalipofanyika mazungumzo na Serikali iliamuriwa zirudishwe TFF lakini mpaka sasa shirikisho hilo linazifuatilia.

Tangu alipoingia madarakani mwezi mmoja sasa, Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba, ni lazima TRA ikusanye kodi ipasavyo na mamlaka nyingine kama bandari kufanya kazi ipasavyo ili kutoruhusu serikali kukosa mapato yake.

Source;Global

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.