Rais
John Magufuli leo ametimiza mwezi mmoja tangu alipoapishwa kushika
wadhifa huo huku akiweka rekodi ya kuokoa kiasi cha Sh997.4 bilioni
(karibu Sh 1trilioni) ambazo zilikuwa zitumike kwa matumuzi yasiyo ya
lazima, na ukwepaji kodi.
Sh997.4
bilioni zilizookolewa zitaweza kutumika kununua magari ya wagonjwa,
kujenga zahanati, kujenga barabara za lami, kununua madawati, kujenga
vyumba vya madarasa, kuchimba visima, kununua mashine za uchunguzi wa
magonjwa, magari ya wanafunzi, pikipiki kwa maofisa kilimo, mikopo ya
elimu ya juu au kujenga viwanja vya michezo kadri Serikali
itakavyoelekeza.
Dk
Magufuli aliapishwa Novemba 5 katika hafla iliyofana na alianza kazi ya
kutafuta na kuziba mianya ya upotevu wa fedha Novemba 6 alipotembelea
Hazina. Katika mazungumzo ya watendaji wa wizara hiyo Rais Magufuli
alipiga marufuku safari zote za nje na kwamba zitakuwa zinaruhusiwa kwa
kibali maalumu.
Novemba
7 alitembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako aliagiza mashine
za MRI na CT-Scan zitengenezwe na aliagiza Sh3 bilioni zitolewe
kugharimia matengenezo kati ya Sh7 bilioni zilizokuwa zinahitajika.
Novemba
19, Dk Magufuli aliwasilisha bungeni jina la Kassim Majaliwa, mbunge wa
Ruangwa kwamba ndiye alimpendekeza kuwa Waziri Mkuu. Baada ya jina
kupitishwa na Bunge, Novemba 20 Kassim Majaliwa aliapishwa.
Jioni
alilihutubia Bunge akionyesha mwelekeo wa Serikali yake ya awamu ya
tano. Katika hotuba hiyo iliyowasisimua wabunge na hata wananchi
waliosikiliza kupitia televisheni na redio, Dk Magufuli aliahidi
kupambana na mafisadi, kubana matumizi, kuhimiza utendaji kazi, kuinua
uchumi na kulinda amani na utulivu.
Baada
ya hapo Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa wamekuwa wakitembelea maeneo
muhimu kwa uchumi wa nchi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bandari
na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL)
Utendaji
huo wa Serikali wa Magufuli ndani ya mwezi moja na kipindi kabla
hajaunda baraza la mawaziri, umetazamwa na jamii kuwa ni mbinu ya
kusafisha nchi na kutengeneza mazira safi ili mawaziri watakaoteuliwa
wafuate kasi hiyo.
Fedha zilizookolewa
Kwa
kuzingatia ripoti ya matumizi ya fedha za safari zilizolipwa kama nauli
na posho kwa kipindi cha kati ya mwaka 2013 na 2015 kiasi hicho ni
pamoja na Sh356.3 ambazo zingeweza kutumika kwa safari hizo. Dk Magufuli
aliagiza kwamba baadhi ya shughuli zitafanywa na mabalozi wa Tanzania
walioko nje.
Novemba
19 alipozindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma, Dk
Magufuli aliagiza Sh225 milioni zilizokuwa zimekusanywa kwa ajili ya
hafla ya wabunge, zipelekwe kununua vitanda katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili. Fedha hizo zilinunua vitanda 300, magodoro 300, mablanketi
1675, na viti vya magurudumu 30.
Pia,
katika hotuba yake bungeni, Dk Magufuli alirejea uamuzi wake wa kufuta
safari za nje kwa watendaji wa Serikali na kueleza safari hizo
zimeigharimu Serikali Sh356.3bilioni ambazo zingeweza kujenga barabara
ya lami yenye urefu wa kilomita 400.
Novemba
23, Dk Magufuli alitangaza kufutwa kwa maadhimisho ya Siku ya Uhuru
Desemba 9 na akaagiza Sh4 bilioni ambazo zingetumika zitumike kufanya
upanuzi wa barabara ya Morocco kwenda Mwenge. Kazi hiyo imeanza.
Novemba
25, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alitangaza kufutwa
maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani na akaelekeza kwamba fedha
zilizopangwa kwa ajili ya sherehe hizo zitumike kununua dawa za kufubaza
makali ya ukimwi (ARVs).
Novemba
27, Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea bandarini na kubaini makontena 349
ambayo yalitolewa bandarini bila kulipiwa ushuru na kuifanya Serikali
kukosa mapato ya Sh80 bilioni.
Tayari
wenye makontena hayo wameanza kulipia na jana TRA ilitangaza kukusanya
Sh6.3 bilioni kati ya hizo Sh80 bilioni. Katika ziara yake nyingine ya
kushtukiza Desemba 3 Majaliwa alibaini makontena 2,431 yalitolewa bila
kulipiwa kodi. Ikiwa makontena hayo yangelipiwa kodi viwango sawa na
yale 349 Serikali ingepata Sh557.2 bilioni.
Desemba
3, Dk Magufuli alifanya mazungumzo na jumuiya ya wafanyabiashara nchini
na akawataka wote ambao waliondoa mizigo yao bandarini bila kulipa
kodi, wajitahidi kulipa katika kipindi cha siku saba kuanzia juzi
vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Makontena ni shida
Desemba
1, makontena mengine tisa yalikamatwa na TRA eneo la Mbezi, Tangibovu
yakiwa yametoroshwa bila kulipuiwa ushuru wa Sh58 milioni. Jumla ya
Sh637.2 zimeokolewa kutokana na mkakati wa kukusanya fedha kutoka kwenye
makontena 2,431 pamoja na 349 na hayo tisa.
Matumizi ya Sh 997.4 bilioni
Kwa
muda mrefu, Serikali imekuwa ikikwama kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo kutokana na kukosa fedha. Dk Magufuli alikiri juzi kuwa hakuna
fedha za maendeleo zilizokuwa zimetolewa kwa wizara zote katika mwaka
huu wa fedha wa 2015/16, lakini baada ya miezi sita juzi ndiyo
zimetolewa Sh120 bilioni.
Dk
Magufuli hakusema Serikali imepata wapi fedha hizo, lakini huenda ni
sehemu ya fedha ambazo ameokoa katika kipindi cha mwezi mmoja.
Kama
fedha hizo zingeelekewa katika ujenzi wa barabara, na kwa kuzingatia
kilomita moja inajengwa kwa Sh1 bilioni, fedha hizo zitaweza kujenga
karibu au zaidi ya kilomita 1,000, ambao ni umbali kutoka Dar es Salaam
hadi Kigoma au Dar es Salaam mpaka Tunduma.
Aidha,
Sh997.4 bilioni zingeweza kununua magari 3,325 ya kubebea wagonjwa kwa
gharama ya Sh300 milioni kwa kila moja na kuwezesha kila mkoa kupata
magari 133 ya aina hiyo.
Pia,
zahanati moja yenye vifaa vyote muhimu ujenzi wake unagharimu kati ya
Sh600 milioni na Sh700 milioni. Hivyo, fedha hizo zingeweza kujenga
zahanati 1,425 yaani kila mkoa ungepata zahanati 57.
Vilevile,
wakati maelfu ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wanasoma kwa
kukaa chini kutokana na kukosa madawati, Sh997.4 bilioni zitaweza
kutengeneza madawati yenye miguu ya chuma 33,249,142 kwa gharama ya
Sh30,000 kwa kila moja na kuwezesha kila mkoa kupata madawati 1,329,966.
Pengine,
fedha hizo zinaweza kujenga vyumba vya madarasa 132,996 kwa bei ya
Sh7.5 milioni kwa darasa moja, hatua ambayo itawezesha kujengwa kwa
vyumba vya madarasa 5,319 kila mkoa nchini.
Kipimo
maarufu cha CT-Scan ambacho ufanyaji wake wa kazi unasuasa Muhimbili
kwa muda mrefu, kinauzwa kwa wastani wa Sh900 milioni, hivyo, Sh997.4
bilioni zitaweza kununua mashine 1,108 ambazo zingesambazwa na kila mkoa
ukapata mashine 44.
Gharama
za kuchimba kisima kifupi ni kati Sh1 milioni na Sh3 milioni kulingana
na jiografia ya eneo husika, hivyo Sh997.4 bilioni zitaweza kuchimba
visima 332,491; kila mkoa ukapata visima 13,299.
Pia,
kwa kuwa Serikali inahimiza uboreshaji wa sekta ya kilimo, Sh997.4
bilioni zitaweza kununua pikipiki 332,491 na kugawiwa kwa maofisa kilimo
kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa kilimo vijijini na kila mkoa
ungepata pikipiki 13,299.
Kama
fedha hizo zitaelekezwa kwenye mikopo ya elimu ya juu, zitaweza
kugharamia wanafunzi 249,368 wa mwaka wa kwanza kwa asilimia 100 kwa
wastani wa Sh4 milioni kwa kila moja kwa ajili ya chakula, malazi na
ada.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Joyce Mmasi na Peter Saramba
0 comments:
Post a Comment