RAIS John Magufuli amesikitishwa na uzushi unaofanywa kwa lengo la kumchafua Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na familia yake, na amewataka waandishi wa habari na vyombo vya habari kuacha kuandika na kuchapisha taarifa za uzushi na badala yake vizingatie weledi na kufuata sheria.Amesema taarifa zinazomhusisha kwamba amezuia mizigo ya mke wa Rais mstaafu Kikwete, Mama Salma Kikwete bandarini hadi hapo itakapolipiwa kodi, si kweli na ni uzushi, kwani hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Salma Kikwete.Dk Magufuli aliyasema hayo katika taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baada ya siku za karibuni, baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuchapisha taarifa zinazomhusisha Mama Salma Kikwete na Taasisi anayoiongoza ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwamba imeshindwa kulipia kodi mizigo mikubwa iliyoiingiza nchini na hivyo kuwa hatarini kupigwa mnada.Aidha, taarifa hizo zimemhusisha Rais Magufuli kuwa anahusika kuzuia mizigo hiyo bandarini mpaka hapo itakapolipiwa kodi.“Tunapenda kuutaarifu umma kuwa taarifa hizo si kweli na ni uzushi, kwani Rais Magufuli hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Salma Kikwete,” ilieleza taarifa ya Ikulu.“Rais Magufuli amesikitishwa sana na uzushi huo unaofanywa kwa lengo la kumchafua Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete na familia yake na amewataka waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuacha kuandika na kuchapisha taarifa za uzushi na badala yake vizingatie weledi na kufuata sheria,” ilibainisha taarifa ya Ikulu na kuongeza:“Nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa dhidi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mke wake Mama Salma Kikwete, tafadhali wale mnaotengeneza uzushi huu, acheni mara moja na muacheni Rais mstaafu Kikwete apumzike.“Rais mstaafu Kikwete amefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa hili, amestaafu anapumzika, narudia muacheni apumzike, Serikali haitaendelea kuvumilia uzushi na uchonganishi huu unaofanywa kwa makusudi ili kuwachafua viongozi wastaafu,” ameonya Rais Magufuli.Mwishoni mwa wiki, WAMA ilikanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki kwa lugha ya Kiswahili kuwa Mwenyekiti wake, Mama Salma Kikwete ana mzigo mkubwa bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi.Taarifa ya Wama iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wake, Daudi Nassib, ilisema taarifa hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gazeti hilo lilichapisha habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari, “Mali za Salma Kikwete kuuzwa kwa mnada?” Katika toleo lake hilo la Novemba 30, mwaka huu,“Kumetolewa madai eti kwamba taasisi ya Wama inayoongozwa na Salma Kikwete inao mzigo mkubwa bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi, hivyo Mamlaka ya Mapato Tanzania imepanga kuuza mali hizo.“Kwa niaba ya Taasisi ya Wama napenda kutoa masikitiko yetu kwamba habari hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote.“Kwa maoni yetu gazeti hilo lina dhamira mbaya dhidi ya Taasisi ya Wama na Mwenyekiti wake Salma Kikwete. Nia yao ni kupaka matope na kuchafua majina na sifa ya taasisi yetu na kiongozi wake.”Katibu Mtendaji huyo alisema ukweli kuhusu jambo hilo ni kwamba, Wama ilitumiwa maboksi 11 ya vitabu vikiwa ni zawadi kutoka Taasisi ya Nakayama ya Japan ambayo ndiyo iliyofadhili ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wama-Nakayama iliyopo Nyamisati, Kibiti na yalishatolewa bandarini tangu Agosti 10, mwaka huu na tayari vitabu viko shuleni na vinatumika.“Hakuna mzigo wowote wa Taasisi ya Wama uliopo bandarini unaosubiri kutolewa wala kuuzwa na TRA,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kulitaka gazeti hilo kuomba radhi kwa Salma Kikwete na kwa Wama kutokana na taarifa hizo.
0 comments:
Post a Comment