Home »
SIASA
» VIGOGO Kutoonekana Sherehe za Uhuru Kwazua Mjadala
Dar es Salaam. Kumekuwa na mjadala wa mahudhurio katika maadhimisho ya sherehe za Uhuru ya mwaka huu ambayo huenda yamevunja rekodi kwa viongozi wengi wa kitaifa na kimataifa kutoshiriki.Licha ya hali hiyo kusababishwa na mambo kadhaa yakiwamo kuingiliana kwa ratiba za shughuli nyingine za kimataifa, ugonjwa na kufiwa kwa baadhi ya viongozi, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamedokeza kuwa huenda imetokana na hatua ya Rais John Magufuli kuahirisha sherehe za mwaka jana.Lakini juzi, Rais Magufuli alitumia Sherehe za Miaka 55 ya Uhuru kueleza sababu, “Kwanza sherehe za mwaka jana ilibidi tusiadhimishe kama zilivyopangwa kwa sababu mbili; sababu ya kwanza zilikuwa zifanyike mwezi mmoja tu baada ya kuapishwa, kwa hiyo hata baraza langu na watendaji wangu wengine nilikuwa bado sijawateua.“Lakini sababu ya pili, nilipoambiwa gharama za sherehe hizo mwaka jana zilikuwa (shilingi) bilioni nne, nikawa ninajiuliza bilioni nne kuna mambo yapi yatafanyika? Itakuwa ni kualika wageni, kutakuwa na chakula, kutakuwa na posho na kadhalika.”Alisema alipouliza hizo posho na chakula wangekula Watanzania wote, akajibiwa kuwa ni kwa ajili ya wale tu walioalikwa, akaamua fedha hizo ziende kupanua Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ambayo inapitiwa na Watanzania wengi.Alisema ameamua sherehe za mwaka huu zifanyike kwa sababu gharama zake zimepungua kwa kuwa ziliishia palepale uwanjani, tofauti na siku nyingine ambazo Rais huandaa dhifa ya Taifa ambayo hufanyika Ikulu jioni.Katika sherehe hizo, marais wawili wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kati ya watatu waliopo hawakuhudhuria kadhalika na Mama Maria Nyerere ambaye ni mjane wa Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanzania na mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli.Pia, mawaziri wakuu wastaafu wote waliopo; Jaji Joseph Warioba, Dk Salim Ahmed Salim, John Malecela, Cleopa Msuya, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo Pinda hawakuonekana.Mbali ya hao, viongozi wote wa mhimili mwingine wa Dola, Spika wa Bunge, Job Ndugai na naibu wake, Dk Tulia Ackson pia hawakuwapo. Aidha, tofauti na sherehe kama hizo miaka ya nyuma, juzi hakuna mkuu wa nchi yoyote ya nje aliyehudhuria wakiwamo wa Afrika Mashariki.Matukio hayo pamoja na lile la Rais Magufuli kutambua uwepo wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa bila ya kumtaja Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita aliyekuwapo, yameibua mjadala mkubwa katika viunga mbalimbali na mitandao ya kijamii baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.Sababu za kutohudhuriaAkizungumzia kutohudhuria kwa viongozi hao, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Hassan Abbas alisema kwa kawaida viongozi wote wa kitaifa hualikwa na hata katika sherehe za juzi, walialikwa bila kujali wanatoka chama gani.Licha ya Abbas kutofafanua, Lowassa na Sumaye huenda hawakufika katika sherehe hizo baada ya kukihama chama tawala, CCM na kujiunga na Chadema mwaka jana ambako Lowassa aligombea urais huku Sumaye akiwa mpiga debe wake mkubwa. Alishika nafasi ya pili nyuma ya Rais Magufuli.“Kama mtu hajafika, muwaulize kwanini hawajafika mimi siyo wa kujibu hilo, ila viongozi wote walialikwa,” aliongeza.Kuhusu kutokuwapo kwa viongozi wa mataifa ya nje, Abbas alisema, “Sidhani kama walialikwa lakini hilo linasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, na ‘statement’ (taarifa) ilitoka, muulizeni Waziri Jenista Mhagama.”Hata hivyo, Waziri Mhagama hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo lakini katika taarifa yake kuhusu maandalizi ya sherehe hizo hakuzungumzia lolote juu ya wakuu wa mataifa mengine kuhudhuria.Hata hivyo, licha ya kutokuwapo kwa taarifa yoyote rasmi ya kutohudhuriwa kwa baadhi ya viongozi wa kitafa imeelezwa kwamba Mkapa alikuwa Burundi katika utatuzi wa mgogoro wa kisiasa nchini humo na Kikwete alikuwa Msumbiji akihudhuria mkutano wa kimataifa uliokuwa ukijadili uwekezaji katika fursa za kielimu.Pia Rais huyo wa Awamu ya Nne alituma salamu za Uhuru kwa Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa Twitter akiwa Maputo, Msumbiji akisema: “Salamu za heri ya kumbukumbu ya miaka 55 ya uhuru wetu, kwetu sote na kwa Amiri Jeshi Mkuu, mheshimiwa Rais.”Aidha, Pinda hakuhudhuria pengine kutokana na msiba wa baba yake mzazi, Xavery Mizengo Pinda (90) aliyefariki mwishoni mwa mwezi uliopita katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.Kadhalika, Mzee Malecela hakuhudhuria pengine kutokana maradhi na Agosti Rais Magufuli alimtembelea kumjulia hali yeye na Spika Ndugai.Maoni ya wachambuziAkizungumzia kutokuwapo kwa viongozi wa nje hasa mataifa ya jirani, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema hilo linaleta maswali mengi katika jamii. Pia alisema ilikuwa ni jambo muhimu kwa viongozi wote wa kitaifa kuwapo uwanjani ili umoja na mshikamano unaohubiriwa majukwaani, uanze kuonyeshwa kwa vitendo na viongozi wenyewe katika tukio hilo muhimu kwa historia ya Taifa.“Tunaposema Tanzania ina umoja na mshikamano lazima tuanze kuuona kwa viongozi wenyewe, wastaafu walipaswa kuwapo au la tuambiwe sababu za msingi za kutokuwapo kwao,” alisema.Alisema alitarajia kuona sherehe hizo zikipambwa na marais kutoka nchi za jirani ikiwamo za Afrika Mashariki jambo ambalo halikutokea.Sanga alionyesha wasiwasi wake kwamba huenda uamuzi wa Rais Magufuli wa kuadhimisha sherehe hizo kwa kufanya kazi mwaka jana, umewafanya viongozi wengine wa nchi za jirani kusita kuhudhuria.“Urais ni taasisi hivyo, kama mwaka jana tuliadhimisha kwa kufanya kazi basi msimamo huo ungeendelea kwa sababu naamini kulikuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo. Kwa mtazamo wangu, naona huenda jambo hilo limechangia sherehe hizi kukosa uwakilishi wa nchi za jirani hata zile ambazo Tanzania ilizisaidia kutafuta uhuru wake,” alisema.Alisema ipo haja kwa Serikali kulijulisha Taifa ikiwa ilitoa mialiko kwa viongozi hao au haikutoa na sababu zake kuondoa sintofahamu iliyopo.Profesa wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alizungumzia kutokuwepo kwa viongozi wa kitaifa ya nje na kusema hakuna mushkeli wowote.“Hicho siyo kiashiria kwamba kuna mushkeli, Tanzania bado imeshikamana, hao viongozi wengine kama Rais mstaafu Kikwete najua yuko nje ya nchi lakini mkewe alikuwepo. Labda swali la kujiuliza kwa nini Lowassa na Maalim Seif Sharif Hamad hawakuwepo? Tanzania hii ni yetu sote, uhuru ni wetu, walipaswa kuwepo. Lakini bado sioni mushkeli, Tanzania bado ni moja,” alisema.Kauli ya Profesa Bana iliungwa mkono na Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (Rucu) Iringa ambaye alisema hakuna tatizo kwa viongozi hao kutohudhuria kwani huenda walikuwa na dharura.Alisema katika hotuba yake, Rais Magufuli aliwataja kwa majina viongozi wastaafu akiwashukuru kutokana na mchango wao katika kulifikisha Taifa mahali lilipo tangu Tanzania ilipopata Uhuru.“Inawezekana tu walikuwa na shughuli nyingine, si muhimu wote kuwepo tulichukulie suala hili hivyo lilivyo,” alisema.Hata hivyo, Profesa Mpangala aligusia suala la mgogoro wa CUF, hasa Rais Magufuli alipomtaja Profesa Lipumba aliyekuwapo uwanjani wakati wa sherehe hizo, kwamba inaonyesha anautambua uenyekiti wake wa chama hicho.“Mimi nilitafsiri kwamba, Rais Magufuli anamtambua kama mwenyekiti wa CUF japo ni ukweli ni kwamba, uenyekiti wake una utata. Mtu alijiuzulu na kurudi tena, hii si sawa,” alisema.Alisema kutambuliwa kwa Profesa Lipumba kama kiongozi wa chama cha siasa kunadhoofisha upinzani Zanzibar na Bara.“Kunamdhoofisha Lowassa huku Bara na Maalim Seif kule Zanzibar kwa sababu inaonekana nyuma yake kuna sapoti ya wazito,” alisema
0 comments:
Post a Comment